Mradi mkubwa wa ujenzi wa Daraja la Kisasa linalojengwa katika eneo la Kigamboni Jijini Dar es salaam unatarajiwa kuanza kutoa huduma rasmi Mwezi Julai mwaka ujao wa 2015 baada ya kukamilika ujenzi wake mwezi wa June mwaka ujao.

Meneja mradi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } Mhandisi Karim Mattaka alieleza hayo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara maalum kukagua ujenzi wa Miradi mikubwa inayogharamiwa na mfuko huo.

Miradi hiyo muhimu kwa ustawi wa jamii ni pamoja na Daraja hilo la Kigamboni na Nyumba za Mkopo Nafuu zinazojengwa katika eneo la Kijichi Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es salaam.

Mhandisi Mattaka alisema miradi hiyo inayokwenda sambamba ujenzi wake itakapokamilika itasaidia kupunguza msongamano wa wasafiri wa maeneo hayo pamoja na makaazi hasa vijana wanaoanza ajira mpya katika taasisi mbali mbali za umma.

Meneja Mradi huyo wa NSSF alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujenzi huo uliofikia hatua ya zaidi ya asilimia 60% unafanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi wa Madaraja kutoka Jamuhuri ya Watu wa China { China Mager Bridges }.

Alifahamisha kwamba Daraja hilo lenye urefu wa nusu Kilomita litakuwa na bara bara mbili zenye uwezo wa kupitisha magari matatu kwenye njia tatu kwa wakati mmoja kwa kila bara bara.

Aliongeza kwamba wajenzi wa mradi huo hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa nguzo 13 zinazokwenda sambamba na ujenzi wa Mnara utakaokuwa na ghorofa 30.

Alieleza kuwa zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni Mia mbili ya Kumi na Nne zitatumika katika ujenzi huo ambapo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } imechangia asilimia 60% wakati Serikali Kuu imechangia Asilimia 40%.

Balozi Seif akiambatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi alieleza faraja yake kutokana na kasi ya mradi huo ambao utajenga Hiostoria ta Tanzania inayokwenda na mabadiliko ya kasi ya Sayansi na Teknolojia.

Balozi Seif aliyapongeza Kampuni ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa juhudi zinazochukuwa za kupelekea kupata fursa kubwa ya kuaminika ndani ya Bara la Afrika kwa kufikisha taaluma waliyonayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akaangalia harakati za ujenzi wa nyumba za mkopo nafuu zilizo chini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } zilizopo Kijichi Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es salaam.

Meneja Mradi wa NSSF anayesimamia ujenzi wa nyumba Hizo Mhandisi Msemo alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi wa nyumba hizo hivi sasa uko katika awamu ya Pili unashughulikiwa nyumba za ghorofa.

Mhandisi Msemo alisema awamu hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka ujao na kufuatiwa na ule wa awamu ya tatu utakashughulikia ujenzi wa nyumba za Watu Mashuhuri { VIP }.

Alisema mradi huo hivi sasa unakabiliwa na changamoto ya huduma za maji safi na salama pamoja na umeme hali ambayo Mfuko huo umelazimika kuchimba visima sita vitakavyosaidia kuondosha tatizo hilo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania kwa mpango wake wa kujenza nyumba za mkopo nafuu.

Balozi Seif alisema huo ni mpango unaotoa faraja kwani utaweza kuarithisha zaidi Vijana wanaoanza ajira katika miaka ya hivi sasa ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa makaazi bora ya kuishi.

“ Tunashukuru kuona kwamba fedha zetu za michango tunazokatwa katika mishahara yetu mnazitumia vizuri na makini katika kuwekeza kwenye miradi inayotambulika na kila mwana jamii “. Alisema Balozi Seif.

Balozi alifanya ziara hiyo maalum yha kukagua miradi hiyo mbali ya kuwa kiongozi wa Serikali lakini pia yeye ni mwanachama hai wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF }.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top