Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kujenga mazingira mazuri kwa wastaafu wake ili kustaafu kwao kusiogopwe na kuonekana ni mwanzo wa kuanza kwa kipindi cha maisha ya shida yasiyokuwa na matumaini.

Alisema Serikali inataka kuona wafanyakazi wake wanapopata barua za kustaafu wasianze kuhuzunika kama ilivyozoeleka kwa vile wengi kati yao huhisi kwamba wamefika wakati ambao hawawezi kukopesheka tena kutokana na udogo wa mapato yao wanayopewa kupitia penchezi zao.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akiuzindua Rasmi Mpango maalum ulioandaliwa kwa pamoja kati ya Mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } na Benki ya Posta Tanzania { TPB } wa ukopeshaji uliolengwa kwa wafanyakazi wastaafu wa Mfuko wa ZSSFhafla iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.

Alisema Mpango huu wa utoaji mikopo kwa wastaafu ambao umeshaanza kutekelezwa una lengo la kuleta faraja na kuwasaidia wastaafu katika kukidhi mahitaji yao mbali mbali ya kimaisha.

Mikopo hiyo inayotolewa na Benki ya Posta Tanzania kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar huwasaidia wastaafu kulipia gharama za matibabu, ada za skuli za familia zao sambamba na kuendesha biashara ndogo ndogo zitakazosaidia kupunguza ukali wa maisha ya kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa wale wastaafu wenye sifa za kuomba mikopo hii wajitokeze kwa wingi kwa vile ni fursa muhimu kwao itakayowapa fursa ya kujiendeleza kimaisha.

Aidha Balozi Seif pia aliwaomba wastaafu watakaochukuwa mikopo kwa kufanya biashara kuhakikisha kuwa biashara wanazotaka kuzifanya wanazielewa vizuri ili kuepukana hasara sambamba na kukumbuka kuwa mkopo lazima ulipwe kupitia pencheni zao na kurejeshwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja hadi miaka mitatu kulingana na umri wa mwombaji.

“ Hakika mpango huu ni mkombozi kwa mstaafu na pia utasaidia Taifa letu kupambana na umasikini wa kipato. Matarajio yangu kuona wastaafu wanatumia fursa hii ili kuweza kujiendeleza kimaisha kwa kuwekeza kwenye miradi yenye faida nzuri “. Alisema Balozi Seif.

Balozi Seif aliushukuru Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar pamoja na Benki ya Posta Tanzania kwa kubuni mpango maalum wa kutoa mikopo kwa wastaafu ili waweze kuishi maisha yenye matumaini.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania Bwana Sabasaba Moshingi alisema kwa muda mrefu sasa taasisi mbali mbali za fedha hapa nchini zimekuwa hazitoi mikopo kwa wastaafu kwa dhana kwamba hawana 

Bwana Sabasaba alieleza kwamba Benki ya Posta kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ililiona tatizo hilo baada ya kutambua mchango mkubwa uliotolewa na wastaafu hao wakati wa utumishi wao na kufikia uamuzi wa kubuni mpango huo ambao ni mkombozi kwa wastaafu hao.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Benki ya Posta alisema kwamba utafiti uliofanywa unaonyesha wazi kwamba wastaafu wamekuwa wakiingiza kiasi kikubwa cha fedha katika uchumi kutokana na mafao wanayolipwa.

Alifahamisha kwamba mafao hayo yanaweza kuleta athari katika Nyanja za kiuchumi, kuongeza ajira, kukuza kipato na kupunguza umaskini iwapo fedha hizo zitatumika kwa busara na kuwekezwa katika maeneo salama.

Bwana Sabasaba amezishawishi taasisi za kifedha ikiwemo Mabenki na wataalamu wa uwekezaji na fedha kubuni njia mbali mbali za kuwasaidia wastaafu ili waweze kuwekeza na kuendelea kufurahia maisha ya ustaafu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khamis Filfil Thani alisema mafao ya wastaafu muda mwingi huongeza mapato ya Taasisi za fedha na kuleta utulivu kwa wastaafu.

Nd. Filfil Thani alieleza kwamba mzunguuko wa mafao ya wastaafu katika taasisi mbali mbali za kifedha Nchini Tanzania umefikia Shilingi Trilioni Mbili wakati ule unaosimamiwa na ZSSF uliohusisha wastaaf 4,000 umepindukia shilingi Bilioni 20.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii aliwaomba wale wasio wanachama wa mfuko huo wako huru kujiunga licha ya kwamba wengi wa wanachama wake ni watumishi wa umma na baadhi ya taasisi binafsi.

Alieleza kwamba Mfuko huo hivi sasa tayari unatumia mipango miwili ule wa lazima kwa watumishi wa umma pamoja na ule wa hiyari ambao Mtanzani ye yote yuko huru na anafusa zote za kujiunga wakati wowote.

Mikopo Maalum ya wastaafu wa mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar inayotolewa tayari imeshafaidisha wanachama wastaafu wapatao 250 kupitia mpango huo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Hafla hiyo ya uzinduzi wa mpango Maalum wa Mikopo kwa wafanyakazi wastaafu wa Mfuko wa hifadhi ya Jamii ilifuatiwa na futari ya pamoja iliyoshirika washiriki wote wa hafla hiyo.

Futari hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View pia ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa taasisi za Kidini na baadhi ya watu maarufu hapa Nchini.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top