Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amewathibitishia Wana CCM, Wananchi na Jamii kwamba ataendelea kufuatilia matatizo na changa moto zinazowakabili wananchi popote pale akiwa kama mtendaji Mkuu wa Serikali.

Alisema Wanasiasa wasifikirie kwamba anapokwenda majimboni hasa katika maeneo yanayoongozwa na Upinzani wakadhani ya kuwa anakwenda kuvuruga siasa za vyama vyengine vya upinzani.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wana Maskani ya CCM ya Amani na Utulivu iliyopo katika Kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja akitekeleza ahadi waliyoitoa yeye na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dr. Ali Moh’d Sheni katika ziara yao ya Tarehe 2 Mei Mwaka 2013 ya kujenga Maskani hiyo katika hadhi ya kisasa.

Akikabidhi mchango wa shilingi Milioni 4,000,000/- zitakazotumika katika ujenzi wa Maskani hiyo Balozi Seif alisema bado ana wajibu wa kufanya hivyo kwa vile yeye ni kiongozi wa Serikali na Siasa.

Alifahamisha kwamba anachokifanya muda wote ni kuangalia shida na kero zinazowakabili Wananchi na kutafuta mbinu za kuzikwamua na zile zilizo nje ya uwezo wake huziwasilisha Serikalini kwa hatua zaidi ya kutafutiwa ufumbuzi muwafaka.

Aliwashangaa baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaoendelea kumshutumu kwa kitendo na uamuzi wake wa kufuatilia kero, matatizo na changamoto hizo zinazowakabili wana jamii katika maeneo yao mbali mbali hapa Nchini.

“ Hivi nikuulizeni Wananchi, ni kweli hamuhitaji huduma za maji zinazoletwa na Serikali ? Kweli hamuhitaji hudum za umeme zinazotengenezewa miundo mbinu na Serikali ambazo baadhi ya wanasiasa zinawakera ? “ Aliuliza Balozi Seif.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba wananchi wasibabaishwe na maneno ya wanasiasa wasiowatakia maendeleo yao.

Mapema akitoa Taarifa fupi ya wana Maskani hao wa CCM wa Amani na Utulivu ya Nungwi Katibu wa Tawi la CCM la Kijiji hicho Nd. Adibu Ali Sheha alisema wana maskani hao wamepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Ilani na Sera za CCM tokea kuanzishwa kwake.

Ndu. Adibu alisema licha ya utekelezaji huo wa sera za CCM lakini wana Maskani hao wapatao 85 hivi sasa pia huendesha miradi ya kujiongezea mapato kwa kujishughulisha na kazi za mikono ikiwemo ushonaji wa mikoba, mikeka makawa na charahani.

Hata hivyo Nd. Adibu alieleza kwamba wana maskani hao wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa mashine ya kudarzi ili kufanikisha kazi zao tatizo ambalo Balozi Seif alilichukuwa na kuahidi kulifanya kazi.

Baadaye Balozi Seif alipata fursa ya kukagua pango kubwa la maji liliopo katika Kijiji cha Mvuleni ambalo Wananchi wa Kijiji hicho hulitumia kwa kupata huduma za maji licha ya kwamba baadhi ya msimu maji hayo huchaganyika na maji ya chumvi kutegemea kima cha maji ya bahari .

Balozi Seif alishuhudia changamoto kubwa inayowapata wananchi hao hasa akina mama ya kusaka huduma hiyo muhimu kwa kulazimika kuteremka na kupanda mlima mkubwa uliopo pembezoni mwa pango hilo.

Balozi Seif pia aliangalia jengo la Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji cha Mvuleni na kuwaagiza waumini wa Msikiti huo kumtafuta fundi atakayefanya tathmini ya makisio ya kujengwa upya kwa paa, vyoo na sehemu ya nyongeza ya nje ili kuwapa utulivu wa ibada waumini hao.

Akizungumza na Wananchi hao mara baada ya ziara hiyo fupi Balozi Seif aliwahakikishia kwamba Wahandisi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar wanajiandaa kuliondosha tatizo la huduma za maji safi katika Kijiji hicho.

Alisema wahandishi hao wamethibitisha kwamba huduma za maji safi na salama zinatarajiwa kupatikana ndani ya Kijiji hicho katika kipindi cha miezi mitatu kupitia kisima cha maji kiliopo Kigongoni.

Aliwaeleza wananachi hao kwamba Mamlaka ya Maji Zanzibar haijapuuza wazo lao la kuchimbiwa kisima chao ndani ya Kijiji hicho, lakini kinachohofiwa na wataalamu hao ni mazingira ya maji katika eneo hilo ambayo baadhi ya wakati huchanganyika na maji ya chumvi.

Katika kuunga mkono juhudi za Mamlaka ya Maji Zanzibar za kuwapatia maji safi na salama wananchi hao wa Kijiji cha Mvuleni Balozi Seif aliahidi kuchangia shilingi Milioni 5,000,000/- zitakazoongeza nguvu za utekelezaji wa kazi hiyo.

Naye Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mama Asha Suleiman Iddi aliwatanabahisha akina mama wa Vijiji hivyo kujiepusha na ushawishi wa vurugu za wanasiasa ambazo hatma yake huzaa matatizo yasiyokwisha.

Mama Asha alisema dunia imekuwa ikiendelea kushuhudia madhila na maafa yanayowapata wanawake na watoto hasa katika maeneo yanayozunguukwa na migogo ya kisiasa pamoja na vita.

Mapema Balozi Seif alikabidhi Fedha Taslimu shilingi Milioni 1,600,000/- kwa Vikundi vya Hiari ya Moyo, Hatuyumbi Maskani, Vijana wa Dufu pamoja na Vijana wa CCM wa kijiji hicho waliopatiwa pia sare za CCM ambapo kila kikundikatika mgao huo kimepata shilingi Laki 400,000/-.

Balozi Seif pia akakabidhi Futari, mashafu, Juzuu kwa wananchi wa Kijiji cha Mvuleni pamoja na Seti ya Jezi kwa timu ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi wa Kijiji hicho.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top