Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwa na wajibu na jukumu kubwa la kuwatunza na kuwathamini wazee wasiojiweza hivi sasa kutokana na mchango wao mkubwa walioutoa kwa nchi hii wakati wa kulitumikia Taifa lao.

Alisema mchango wa wazee hao umekuwa ukiendelea kutumiwa na wananchi walio wengi hapa nchini ikiwemo kigezo cha amani na utulivu kinachotokana na juhudi za wazee hao wakati wa kupigania utu wa mwafrika.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa ziara yake fupi ya kuwasalimia Wazee wanaotunzwa katika Nyumba za Serikali za Welezo na Sebleni na kuwapatia zawadi ya nguo kwa ajili ya kusherehekea vyema siku Kuu ya Iddi El Fitri inayotarajiwa kufanyika mapema wiki ijayo.

Alisema wazee wa Taifa hili wametumia muda wao mkubwa wa kujenga mazingira bora ili kizazi chao kiendelee kuishi kwa amani na furaha tofauti na enzi zao zilizokumbwa na mitihani ya kutawaliwa jambo ambalo liliwakosesha uhuru wa kidemokrasia wa kufanya wanalolihitaji katika maisha yao.

“ Sisi kama Viongozi wa Serikali bado tunathamini na kuheshimuj wazee wetu waliotumia muda wao mkubwa wa kulitumikia Taifa letu kazi ambayo kwa sasa tunafaidika nayo “. Alisema Balozi Seif.

Akigusia suala la mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaahidi Wazee hao wa Welezo na Sebleni kwamba ule utaratibu wake wa kufutari nao pamoja unatendelea kama kawaida penye majaliwa kwa miaka ijayo.

Balozi Seif aliwafahamisha wazee hao kwamba mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani wa mwaka huu ilishindikana kufutari nao pamoja kutokana na kutingwa na majukumu mengi ya kitaifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapatia zawadi ya madira na mitandio yao wazee wa kike na wale wazee wa kiume wakafaidika na kivazi cha asili cha kiko na fulana zake ili wazitumkie siku ya furaha ya iddi el fitri.

Akitoa skurani kwa niaba ya wazee hao wa Welezo na Sebleni Mzee Omar Said alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa juhudi zake za kuendelea kufuatilia changamoto zinazowakabili wazee hao.

Mzee Omar alisema juhudi hizo zimekuwa zikiwapa faraja wazee hao na kuendelea kujenga imani kwa Serikali ambayo inaelewa mchango wao katika ukombozi wa Visiwa hivi.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji,Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto Bibi Asha Abdulla alisema Nyumba za Wazee ziliopo Welezo zimekuwa zikihudumia wazee wapatao 42 ambao kati yao wanawake wapo 14 wakati wazee wa Kiume wanafikia 31.

Kwa upande wa Sebleni Katibu Mkuu Asha alisema Nyumba hizo zinahudumia wazee 46 ambao kati ya hao wazee wa kike wanafikia 29 na wale wa Kiume wapo idadi ya 17 wakiwa chini ya usimamizi wa Idara ya Ustawi wa Jamii iliyopewa jukumu la kuwahudumia wazee hao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top