Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete amewatakia furaha, Baraka na siku kuu njema ya iddi el Fitri Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi wote Nchini Tanzania katika kusherehekea kwa amani baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani.

Rais Kikwete alitoa salamu hizo katika futari ya pamoja aliyowaandalia wananchi wa Mikoa Mitatu ya Unguja zilizowakilishwa na kuwasilishwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Futari hiyo ya pamoja ikiwa ni utaratibu wake anaoendelea kuufanya kila mwaka kwa waumini na wananchi wa mikoa mbali mbali hapa Zanzibar ndani ya kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani ilifanyika katika ukumbi wa Salama uliopo Bwawani Mjini Zanzibar.

Alisema waumini hao pamoja na wananchi wote wanapaswa kuzingatia amani na utulivu uliopo nchini katika kusherehekea siku kuu hiyo kwa upendo kama vitabu vya dini na maagizo ya viongozi wanaosimamia dini wanavyoshauri na kusisitiza kila mara.

Alielezea matumaini yake kwamba jamii itaendelea na harakati zake za kimaisha katika kuyaendeleza yale yote iliyojifunza ndani ya mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani katika misingi ya haki, wajibu, upendo na kuaminiana.

Mapema Waziri wa Katiba na sheria Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakari akimkaribisha Balozi Seif kwenye hafla hiyo alisema mwenye kumfutarisha mwenzake ndani ya ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa ramadhani mtu huyo hupata fadhila kubwa kutoka kwa mola wake.

Waziri Aboubakar alieleza kwamba utaratibu wa kufutari pamoja miongoni mwa waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi husaidia kujenga umoja na mshikamano ndani ya mioyo kutokana na mkusanyiko huo miongoni mwa watu hao.

Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini na wananchi hao wa Mikoa Mitatu ya Unguja waliopata bahati ya kuhudhuria futari hiyo ya pamoja Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi alimpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uamuzi wake aliochukuwa wa kuwakutanisha wananchi katika futari ya pamoja.

Mh. Abdulla Mwinyi alisema kitendo hicho chema na kinachopaswa kuigwa na baadhi ya wengine wenye uwezo wa kufanya hivyo kinasaidia kuzaa fikra zinazowapa muelekeo wale waliokusanyika pamoja katika kubuni mipango na maarifa yanayowapa muelekeo mzuri katika mambo yao ya baadae.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ameshawahi kuandaa Futari kama hiyo mapema wiki hii kwa waumini na Wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba iliyofanyika kwenye majengo ya Ikulu ya Serikali ya Jamuhuri iliyopo Mjini Wete Pemba.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top