Mzee aliyepigwa mapanga na mtoto wake kwa madai ya kumyima daku kijana huyo, ameelezea jinsi alivyopatwa na mkasa huo usiku wa manane wakati wakijiandaa kula daku.
 
Mzee huyo Gharib Amour Khamis (60) mkaazi wa Tumbe Wilaya ya Micheweni, ameelezea mkasa huo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefika nyumbani kwake kumjuilia hali ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea wagonjwa katika Wilaya hiyo.
 
Mzee Gharib amesema siku kadhaa amekuwa akimuonya mtoto wake huyo Suleiman Gharib Amour (22) kuacha vitendo viovu anavyovifanya ikiwa ni pamoja na kulewa, lakini amekuwa akikataa kuacha vitendo hivyo licha ya kuendelea kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
 
Amesema kabla ya tukio hilo alikuwa akitishia kumnyima daku kwa nia njema akiwa na lengo la kumrekebisha tabia lakini amekuwa hasikii na kuendelea na vitendo hivyo viovu.
 
Amedai kuwa siku ya tukio kijana huyo aliingia ndani usiku wa manane akiwa amelewa na ndipo mzee huyo alipoamuru asipewe daku kwa vile vitendo anavyovifanya ni kinyume cha maadili.
 
Amefahamisha kuwa baada ya kijana huyo kuona kweli amenyimwa daku ndipo alipochukua panga na kuanza kumshambulia kwa mapanga katika sehemu mbali mbali za mwili wake na kumjeruhi zaidi kichwani na mkononi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Shekhan Mohammed Shekhan alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, usiku wa kuamkia Alkhamis ya tarehe 03/07/2014, majira ya saa tisa za usiku.
 
Kamanda Shekhan alisema pamoja na kijana huyo kumjeruhi baba yake mzazi, pia alimjeruhi Mariam Amour Khamis ambao wote walikimbizwa hospitali ya Micheweni kwa matibabu.
 
Baadhi ya wananchi walioshughudia tukio hilo walikiri kuwa kijana huyo alikuwa amelewa chakari na kitendo cha kunyimwa daku ni haki yake kutokana na kwamba huu ni mwezi ya toba.

Taarifa za kipolisi zinasema kuwa kijana huyo ambaye kwa sasa yuko rumande, anatarajiwa kupandishwa kizimbani tarehe 25/07/2014 kwa kusomewa shitaka linalomkabili.
 
Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top