Mheshimiwa Hawa A. Ghasia - Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI,
Mhe. Haji Omar Kheri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ,
Mheshimiwa Abbas H. Kandoro - Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa,
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa,
Katibu Mkuu - Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI,
Prof. Joseph Semboja - Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi,
Naibu Makatibu Wakuu - Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI,
Makatibu Tawala wa Mikoa
Watendaji Waandamizi
Watoa Mada
Wageni Waalikwa
Waandishi wa habari.
Mabibi na Mabwana.

Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa Hotel ya White Sands Dar es salaam katika mafunzo haya ya siku tatu ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ambayo bila shaka ni muhimu sana kwenu pamoja na Taifa kwa jumla.

Naungana na Taasisi ya Uongozi ambao ni waandaaji wa mafunzo haya kuwakaribisha kwenye mafunzo ambayo yatawasaidia watendaji hapa kujikumbusha mambo mbali mbali yanayowahusu ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Aidha naishukuru kwa dhati Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, kwa kunitunukia heshima ya kufungua mafunzo haya ambayo ama hakika maandalizi yake ni ya aina yake.

Ndugu Washiriki wa Mafunzo,

Mafunzo haya yanayoitwa kwa lugha ya kiingereza "Political - Administrative Interface" yameandaliwa mahsusi kuwawezesha kufahamu kwa kina umuhimu wa mawasiliano bora baina ya Viongozi wa Kisiasa ambao ni Wakuu wa Mikoa na Watendaji Wakuu ngazi ya Mkoa ambao ni Makatibu Tawala wa Mikoa ili kuimarisha kwa kiwango cha juu zaidi utoaji bora wa huduma kwa wananchi wetu. 

Naamini, na wengi wanaamini, mmekuwa mkitekeleza kazi na majukumu yenu vizuri lakini kumekuwa na changamoto ya misuguano ya hapa na pale ambayo kwa kiwango kikubwa husababishwa na mawasiliano yasiyoridhisha kati yenu. 

Ni imani yangu kupitia mafunzo haya mtakumbushwa mengi mliyoyasahau, mtapata mengi mapya ya kujifunza, kujikumbusha na kujinoa zaidi. Hayo yafanyika kwa ajili ya kuhuisha uhai wa utekelezaji wa majukumu yetu na pia kuleta mshikamano na umoja miongoni mwa watendaji wetu ili kuepuka misuguano iliyokuwepo.

Ndugu Washiriki wa mafunzo,

Nyinyi ni viongozi ambao mmekabidhiwa dhamana kubwa katika Mikoa yenu ambako ndiko Watanzania wote wanakoishi. Nyinyi ndiyo wawakilishi wa Mheshimiwa Rais katika Mikoa yenu. 

Uwajibikaji na mshikamano wenu ndiyo sababu pekee itakayowezesha watanzania kutimiza wajibu wao wa kuboresha maisha yao. Haya hayatawezekana kama kutakosekana mshikamano katika utekelezaji wa kazi na majukumu yenu. 

Haya hayatawezekana kama hakuna uwazi wa mawasiliano baina ya Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa. Haya hayatawezekana kama kila mmoja wenu kwa maana ya Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa atashikilia msimamo wake akidhani yupo sahihi kuliko mwenzake.

Mafunzo haya yamepewa jina kwa lugha ya kiingereza "Political - Administrative Interface" kwa maana kwamba, Wakuu wa Mikoa ni Viongozi wa Kisiasa na Makatibu Tawala wa Mikoa ni Watendaji Wakuu ngazi ya Mkoa. Kwa muonekano huo basi, mafunzo yameandaliwa ili kuonesha vizuri utekelezaji wa majukumu kwa muingiliano baina yenu.

Ndugu Washiriki wa mafunzo,

Kumekuwa na changamoto ya mahusiano na muingiliano wa kiutendaji miongozi mwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa. 

Hali hii imesababisha baadhi yenu kuamua kufanya anavyoona kwake inafaa na mwisho kila mmoja anawasilisha malalamiko yake ama kwa Waziri Mkuu au kwaWaziri wa Nchi OWM - TAMISEMI au Katibu Mkuu OWM - TAMISEMI. Vitendo hivyo ndivyo vinavyoleta dosari katika utendaji wenu.

Hivyo mahusiano na muingiliano wa utendaji kazi baina ya Viongozi wa kisiasa na watendaji ni muhimu na yanahitajika kwa ajili ya utawala bora na ukuaji wa maendeleo ya Taifa letu. 

Hivyo basi mahusiano baina ya Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa katika utekelezaji wa majukumu ni muhimu, ni kama mtiririko wa uwajibikaji katika sekta ya umma.

Mawasiliano ya Katibu Tawala wa Mkoa kwenda kwa Mkuu wa Mkoa zaidi ni ushauri, maelezo, ufafanuzi na taarifa muhimu, wakati mawasiliano ya Mkuu wa Mkoa kwenda kwa Katibu Tawala wa Mkoa zaidi ni maelekezo ya kisera na uwajibikaji. 

Kwa maana hiyo, pande hizi mbili zinategemeana katika utekelezaji wa ufanisi wa majukumu katika ngazi ya mkoa. Jambo linalohitajika kila mmoja anatakiwa kuwa na imani kwa mwenzake kwa ajili ya kuendeleza uhusiano katika uwajibikaji. Kinyume cha haya Mkoa utakosa mwelekeo kwa sababu kila mmoja atafanya anavyodhani yupo sahihi, na hivyo kusababisha msigano baina yao.

Ndugu Washiriki wa mafunzo,

Uhusiano wa Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa hauishii kwenye utendaji kazi za kila siku bali hata kwenye upangaji wa mipango na upimaji wa utendaji kazi wa nusu mwaka na wa mwaka mzima. Kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Katibu Tawala wa Mkoa husaini na Mkuu wa Mkoa Mkataba wa utendaji kazi ambapo katika tathmini ya mwaka suala la mahusiano ni miongoni mwa vipimo vilivyomo kwenye tathmini hiyo. 

Hapa nimejaribu kuonesha namna ambavyo Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa wanavyohusiana na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao na hakuna namna ambayo watasema hawana mahusiano katika muingiliano wa utekelezaji wa majukumu hayo.

Ndugu Washiriki wa mafunzo,

Mikoa bado inakabiliwa na changamoto za usimamizi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo ndizo msingi wa kutoa huduma bora kwa wananchi. Nyie ndiyo viongozi ambao mnawajibu wa kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja. 

Kwa mfano, wananchi bado wanalalamika kuhusu huduma zisizoridhisha na zisizokidhi viwango zinazotolewa katika Sekta za Umma; bado yapo matatizo ya rushwa; ucheleweshaji wa maamuzi bila sababu za msingi; bado upo ubabaishaji wa baadhi ya watumishi; na bado wapo watumishi wanaokiuka maadili ya Utumishi wa Umma katika ngazi ya Mkoa na kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, na pia wapo watumishi wasiojiamini katika kutoa maamuzi ya haraka na hivyo kusababisha urasimu na ucheleweshaji wa mambo mbali mbali ya maendeleo.

Baadhi ya masuala yanayosababisha kuendelea kwa hali hii ni kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa mawasiliano ya muingiliano wa kiutendaji baina ya Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa.

Ni muhimu sana kwa Viongozi wa ngazi yenu kusimama kwa umoja, mshikamano, mahusiano na uwajibikaji wa pamoja ambavyo kwa ujumla wake mtaonesha picha ya Serikali kwa wasaidizi wenu ambao nao wataiga mfumo wenu wa mawasiliano. 

Mkiwa na misuguano katika utendaji wenu wa kazi halikadhalika watumishi wa chini yenu nao watakuwa na misuguano na matokeo yake kazi hazitaenda badala yake kuwepo kwa mivutano.

Ndugu Washiriki wa mafunzo,

Kwa kuzingatia hilo, sehemu kubwa ya mada zitakazotolewa katika mafunzo haya zitahusu masuala ya msingi ya mahusiano ya muingiliano katika uendeshaji Serikali ambayo nyinyi kama viongozi na watendaji katika ngazi ya Mkoa, ni muhimu sana mkayafahamu.

Nafahamu kuna Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo mbalimbali ambayo mnaitumia katika utendaji wa kazi kama Mkuu wa Mkoa au Katibu Tawala wa Mkoa, lakini kuwepo kwa sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo hiyo hakutowezesha kutekeleza kazi kwa ufanisi iwapo kutakosekana mahusiano mazuri miongoni mwenu.

Nimejulishwa kuwa mafunzo haya yanalenga, kuimarisha mahusiano miongoni mwa Viongozi wa Kisiasa na Watendaji Wakuu na kwa maana hiyo mfumo wa mafunzo ni majadiliano ya pamoja miongoni mwenu.

 Mada zitakazowasilishwa zitahusu namna ambavyo Viongozi na watendaji mnavyoweza kuimarisha mahusiano na kisha majadiliano ya pamoja yatafuata bila kuweka mpaka wa huyu ni Mkuu wa Mkoa, na maadam kasema, basi mimi Katibu Tawala wa Mkoa nikae kimya, hilo halitakiwi na lisiwepo katika mafunzo haya.

Ndugu Washiriki wa mafunzo,

Nimeambiwa kuwa OWM – TAMISEMI, haijawahi kupata nafasi kama hii ambapo Viongozi wa Kisiasa na Watendaji Wakuu wanapata fursa ya kuzungumzia mahusiano yao ya kiutendaji miongoni mwao. 

Nasaha zangu kwenu tumieni nafasi hii kufahamiana vizuri zaidi kama viongozi ili kubadilishana uzoefu na kujenga mtandao wa mawasiliano na mahusiano kwa ajili ya kupashana habari na kushauriana. 

Jengeni mshikamano wa mahusiano katika utendaji kazi wenu. Mkiimarisha maelewano miongoni mwenu mtarahisisha utendaji na kuepusha migogoro isiyo ya lazima. Napenda kuwashukuru Uongozi Institute kwa uamuzi wenu wa kuyaandaa na kuyaendesha mafunzo haya na mkaanza kundi hilo.

Ndugu Washiriki wa mafunzo,

Napenda kumalizia kwa kuwashukuru tena kwa kukubali kuhudhuria mafunzo haya. Nimefarijika kuona mahudhurio yenu ni mazuri. Kwa hivyo basi tumie fursa hii kujadili kwa undani, upana na bila kuogopana ili mkitoka hapa iwe mmezaliwa upya katika suala zima la mahusiano, mawasiliano na muingiliano katika utendaji kazi kwa lengo la kusimamia sera, sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo ya Serikali katika ngazi ya Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mkitoka hapa, naamini mtakuwa kitu kimoja.

Kwa upande wa Taasisi ya Uongozi, naishauri kuona namna ya kuwahusisha katika mafunzo kama haya Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya au Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi na Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, hata kama siyo wote kwa pamoja bali kuyaendesha kwa awamu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika.

Kwa upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Idara Maalum zione namna ya kuwaleta Viongozi wa Halmashauri, Wilaya, Mkoa, TAMISEMI na TAMIM kuhudhuria mafunzo mbalimbali yenye kuboresha uongozi katika maeneo yao kama haya yanayotarajiwa kufanyika leo.

Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ishirikiane na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Idara Maalum (TAMIM) katika kulitekeleza jambo hili.
Mwisho siyo kwa umuhimu, nawaomba watoa mada kutoa muda mwingi katika majadiliano na mashauriano, kutoa mada zenye kulenga kuimarisha mahusiano na mashirikiano baina ya Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa.

Ndugu Washiriki wa mafunzo,

Kwa mara nyingine napenda kuushukuru kwa dhati uongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa kunishirikisha na kujumuika nanyi katika mafunzo haya muhimu.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka kwamba Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yamefunguliwa rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza

0 comments:

 
Top