Chama Cha Wananchi CUF kimesema hakitowavumilia watendaji watakaobainika kuendeleza fitna na majungu ndani ya chama hicho.

Katibu Mkuu wa Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo kwa nyakati tofauti, wakati akizindua kamati tendaji za (CUF) kwa Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Kwa upande wa Unguja mkutano huo ulifanyika ofisi za (CUF) Wilaya ya Magharibi zilizopo Kilimahewa, ambapo mkutano kwa Wilaya nne za Pemba umefanyika ofisi za CUF Wilaya ya Chake Chake.

Akizungumza katika Mikutano hiyo Mhe. Maalim Seif amesema chaguzi kwa ngazi za Wilaya sasa zimekamilika na kuwataka watendaji hao kuendelea kukijenga chama, badala ya kuendekeza fitna na chuki ambazo zinaweza kuwagawa wanachama.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ametangaza rasmi kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho taifa Mzee Machano Khamis Ali hatogombea tena nafasi hiyo kutokana na kuzorota kwa hali ya afya yake.

Hata hivyo amesema Chama kitaendelea kumtunza Mzee Machano kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kukijenga na kukiimarisha chama hicho.

“Mzee Machano ni kisima chetu, na tutaendelea kukitumia hata akiwa nje ya safu ya uongozi wa chama”, alifahamisha Maalim Seif.
Amesema wakati mchakato wa kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa ukiendelea hadi tarehe 10/06/2014, nafasi hiyo iko wazi na yeyote anayetaka kugombea nfasi hiyo yuko huru kufanya hivyo.

Ameelezea kuridhishwa na jinsi chaguzi hizo zilivyofanywa kwa uwazi na kupatikana viongozi waliochaguliwa kwa kura nyingi, licha ya kuwepo upinzani mkali katika baadhi ya Wilaya zikiwemo Wilaya ya Mjini na Micheweni, ambapo chaguzi za Wenyeviti zililazimika kurejewa baada ya kukosekana washindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Mhe. Hamad Massoud Hamad, kwa mara ya kwanza chama hicho kimepata mwenyekiti wa Wilaya mwanamke ambapo wajumbe wa mkutano mkuu Wilaya ya Magharibi walimchagua Bi. Raisa Abdalla Issa kuwa Mwenyekiti wao.

Mhe. Hamad Massoud alisema uchaguzi kwa upande wa Unguja ulikuwa wa aina yake kwani bila ya kutarajiwa wajumbe wa mikutano mikuu Wilaya za Unguja waliwachagua wajumbe 47 wanawake kati ya wajumbe 94 waliochaguliwa, na kufanya idadi sawa katika ya wanawake na wanaume wanaounda kamati tendaji za Wilaya za Unguja.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top