Watendaji wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha mawazo na maagizo yote yaliyotolewa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kikao chao kinachoendelea wanayatekeleza kwa nguvu zao.

Utekelezaji huo ndio kigezo pekee kitakachoashiria Wizara hiyo inafikia lengo liliomo katika mpango wake wa kazi za kawaida na maendeleo iliyouwasilisha kwenye Baraza la Wawakilishi wa mwaka 2014/2015 na kupitishwa na Wajumbe wa Baraza hilo bila ya vikwazo wala kubadilika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo katika dhifa maalum aliyowaandalia watendaji wa Ofisi yake hapo nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar baada ya kazi nzito waliyoifanya ya kuandaa Bajeti ya Wizara hiyo na hatimae kupitishwa na Baraza la Wawakilishi bila ya matatizo.

Balozi Seif alisema kilichokuwa kikiwakabili watendaji hao sio kazi rahisi lakini umoja na mshikamano wao wa pamoja ndio siri halisi iliyochangia kufanikisha kazi hiyo ambayo inafaa kuigwa na Wizara nyengine za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“ Watendaji wa Wizara wamesikia maagizo, ushauri na hata baadhi ya makemeo ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Hivyo kazi iliyo mbele yenu kama watendaji ni kuyatekeleza yote hayo ili kujiweka sawa na Bajet ijayo “. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza watendaji wote walio chini ya Wizara yake na kuwatoa hofu kwamba wako huru wakati wowote kutoa ushauri wao hata mdogo kiasi gani ambao utasaidia na kuchangia kufanikisha majukumu ya Ofisi yao kwa ujumla.

Alisema watendaji wote wa Serikali ni sawa kwa mujibu wa taratibu na kanuni za utumishi Serikalini lakini kilichopo ndani ya utekelezaji wa majukumu ya watumishi husika ni mgawanyo wa madaraka.

“ Niko huru wakati wowote kushauriwa na mfanyakazi ye yote yule bila ya kuona shinda, woga au uzito wowote muhimu ilimradi atakachokishauri kitaleta faida kwa Wizara na Taifa kwa ujumla “. Alisisitiza Balozi Seif.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed amewashukuru Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi kwa mapendekezo yao yaliyoiwezesha Bajeti ya Ofisi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupita bila ya vikwazo.

Waziri Aboud alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba watendaji wa Wizra hiyo wataendelea kumuunga mkono wakati wowote katika utekelezaji wa majukumu yao waliyopangiwa.

Alifafanua kwamba ukaribu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa watendaji na wafanyakazi walio chini ya Ofisi yake kwa kiasi kikubwa umewaondolea woga watendaji hao katika utendaji wao wa kazi za kila siku.

Mapema Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohd kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara hiyo amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Familia yake kwa uamuzi wake wa kuwa pamoja na watendaji wake katika kubadilishana mawazo baada ya kazi nzito ya Bajeti ya Wizara hiyo.

Dr. Khalid alielezea faraja yake kutokana na hamasa kubwa iliyoonyeshwa na wakurugenzi kwa kushirikiana na watendaji wote wa Ofisi hiyo katika kushirikiana pamoja iliyoondoa vikwazo katika uandaaji wa Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka huu.

“ Hamasa iliyoonyeshwa na Viongozi pamoja na watendaji katika kuandaa Bajeti yetu kwa kweli imenipa faraja na kuiwezesha Wizara kufikia malengo mazuri iliyojipangia “. Alifafanua Katibu Mkuu Khalid.

Dhifa hiyo iliyojumuisha watendaji wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi na baadhi ya watendaji wake pamoja na familia ya Makamu wa Pili wa Rais iliongozwa na muziki laini uliokuwa ukiporomoshwa na Kikundi mahiri cha Muziki wa Taarabu asilia cha Akheri Zamani.

Muziki huo ulioongozwa na msanii nguli wa muziki hapa Nchini Matona Issa Matona uliwafanya baadhi ya watendaji hao wakijimwaga uwanjani na kupata burdani mwanana.

Othman Khami Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top