Na: Hassan Hamad (OMKR).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesifu utendaji wa kamati ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Serikali kwa kusimamia vyema majukumu yake na kuleta ufanisi katika ofisi hizo.

Akizungumza katika dhifa maalum kufuatia kupitishwa kwa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ya Mwaka 2014/2015 huko nyumbani kwake mbweni, Maalim Seif amesema kamati hiyo imefanya kazi kubwa ya kuikosoa na kuielekeza ofisi yake hadi kufikia kupitishwa kwa bajeti hiyo.

Amesema kamati hiyo ina wajibu mkubwa wa kusimamia ofisi hizo kiutendaji, na kuitaka kuendelea na kazi hiyo bila ya kuwaonea haya watendaji wa ofisi hizo, ili kuona kuwa zinafanya kazi kwa juhudi na ufanisi zaidi.

Amefahamisha kuwa usimamizi bora wa kamati hiyo ndio unaopelekea ufanisi wa matumizi ya fedha za serikali, na kuwahakikishia wananchi kuwa fedha za walipa kodi zinatumika vizuri.

Aidha Maalim Seif amewashukuru wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kuichambua bajeti ya Ofisi yake na hatimaye kuipitisha kwa kauli moja Jumatatu iliyopita.

Amesema licha ya bajeti ya ofisi hiyo kuwa ndogo, lakini watahakikisha kuwa wanasimamia matumizi ya fedha hizo na kutekeleza malengo waliyojiwekea kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mapema akitoa salamu za kamati hiyo, Mwenyekiti wa kamati Mhe. Hamza Hassan Juma, amesema kamati yake inaridhishwa na utendaji wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, na kwamba imekuwa ikijifunza mambo mengi kutoka kwa watendaji wa ofisi hiyo.

Amewashauri viongozi kupunguza maneno ya kisiasa, na badala yake washirikiane katika kuijenga nchi, na kuwaletea wananchi maendeleo.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Fatma Abdulhabib Fereji amesema mafanikio yaliyopatikana katika ofisi hiyo yanatokana na mashirikiano mazuri ya kiutendaji miongoni mwa watendaji wa Ofisi hiyo.

Amewashauri kuongeza bidii katika utendaji wao, ili kuhakikisha kuwa ofisi inapata mafanikio makubwa zaidi, na kuwawezesha wananchi kupata huduma wanazotarajia kwa ufanisi zaidi.

Kufanyika kwa dhifa hiyo ni utamaduni uliowekwa na ofisi hiyo kila mwaka baada ya kupitishwa kwa bajeti yake.

0 comments:

 
Top