Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema vipaji vilivyoibuka na kushuhudiwa ndani ya mashindano ya mbio za nyika vinafaa kutunzwa na kuandaliwa mazingira ya kuviendeleza zaidi.

Balozi alieleza hayo wakati wa mashindano ya Pili ya Mbio za Nyika { Cross Country } 2014 zilizoanzia mbele ya Skuli ya Sekondari ya Ben Bella Mjini Zanzibar zikiwa za Kilo Mita Nne, Sita na Nane kwa kushirikisha wanafunzi wa msingi na sekondari.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Utyamaduni,. Utalii na Michezo itajitahidi kuwajengea mazingira bora vijana hao wenye vipaji maalum.

Balozi Seif alieleza kwamba michezo hivi sasa imekuwa ajira kubwa na tayari imeshawajengea mazingira mazuri ya utajiri wachezaji mbali mbali wa kimataifa Ulimwenguni.

“ Tumeshuhudia wanafunzi wetu hawa wakionyesha umahiri na vipaji vyao katika mashindano haya kitendo ambacho kitasaidia kuibua vipaji vya wanamichezo chipukizi “. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wanafunzi hao kwa kujikita zaidi katika sekta ya michezo na kuwashukuru wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Filbert Bay ya Mkoani Kibaha kuungana na wenzao katika mashindano hayo.

Ushiriki wa Wanafunzi hao wa Filbert Bay umedhihirisha wazi mshikamano, upendo na udugu uliopo baina ya wanafunzi wa pande mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mashindano hayo Balozi Seif alikabidhi zawadi mbali mbali kwa washindi wa mashindano ya Pili ya mbio za Nyika ambapo Skuli ya Msingi ya Filbert Bay ikionyesha umahiri wake wa ushindi na kiufuatiwa na Skuli ya Ndijani ya Wilaya ya Kati.

Akisoma Risala kwenye mashindano hayo Mkuu wa Kitengo cha Michezo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Maalim Mussa Abdullrabi jumla ya skuli 26 za Sekondari na skuli 21 za Msingi zikijumuisha wanafunzi 485 zilishirikia mashindano hayo.

Mwalimu Mussa Abdullrabi alisema lengo la kuanzishwa kwa Michezo hiyo ni kuitikia agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Shein la kutaka kufufuliwa kwa vugu vugu la michezo mbali mbali hapa Zanzibar.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Michezo Wizara ya Elimu alifahamisha kwamba Wizara hiyo imejipanga kuanzisha Dawati la Michezo litakaloipa fursa Wizara hiyo kushajiisha wafadhili na wadau wa Michezo kusaidia Vifaa klwa ajili ya kuendeleza michezo mbali mbali Maskulini.

Katika mashindano hayo Mbio za Kilomita Nne Wanawake washindi ni Taresia Josephat, Evodia Gabriel na Estar Martin wote kutoka skuli ya Msingi ya Filbert Bay ya Mkoani Kibaha.

Washindi Watatu wa Kilomita Nane ni Idrissa Yussuf wa Skuli ya Mtoni, Salum Pnadu wa Skuli ya Ndijani na Maneno Salim Ali wa Skuli ya Mtoni wakati Kilomita Sta Wanawake washindi walikuwa Regina Deograstius, Doles Contas na Regina Michael wote wa Filbert Bay ya Kibaha.

Kilomita Sita wanaume washindi ni Ibrahim Rashid wa Skuli ya Ndijani, Salha Hamad wa Skuli ya Welezo na Ali Simai Haji wa Skuli ya Ndijani.

Ujumbne wa Mwaka huu katika mashindano hayo ya Mbio za Pili za Nyika { Cross Country } ni “ Acha unyanyasaji, mwache Mtoto acheze kwa usalama” .



Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top