Wazazi na walezi wameaswa kuacha tabia ya kuwaogopa watoto wao, na badala yake wawaongoze katika malezi yenye kufuata maadili mema.

Wito huo umetolewa na mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Awena Sinani Massoud, wakati akizungumza kwenye hafla ya maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), yaliyoandaliwa na Madrasat Azhar ya Tomondo kiziwa maboga.

Amesema tabia iliyozuka kwa baadhi ya wazazi kuwaogopa kuwakanya watoto wao ni hatari, hivyo inapaswa kupigwa vita kwa maslahi ya watoto na taifa kwa ujumla.

Aidha amewaomba wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao katika madrasa, ili kubaini iwapo wanafahamu ipasavyo au wanahitaji nguvu ya ziada katika kuwasomesha.

Mama Awena amesisitiza wajibu wa wazazi kuhakikisha kuwa wale walio chini ya uangalizi wao wanawalea katika misingi ya maadili mema, ili wasipotoke na kupelekea kujihusisha katika vitendo viovu vikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, zinaa na kutojisitiri vizuri hasa kwa vijana wa kike.

Pia Mama Awena amewakumbusha wazazi kuwazoesha watoto kuwa na subra na kutosheka na kile wanachopata kwa mujibu wa uwezo wa wazazi au familia zao.

Amesema iwapo utamaduni huo utaendelezwa, vijana wengi watazoea hali ya maisha waliyonayo, na kuacha tama ya kuiga au kutamani baadhi ya vitu wasivyokuwa na uwezo navyo.

Amewahimiza waislamu kuendelea kuzinduana juu ya mambo ya kheri na yale yanayomchukiza Mwenyezi Mungu, ili kulinda hadhi ya Uislamu duniani, sambamba na kuendeleza mafunzo ya dini hiyo kwa vitendo.

Katika risala yao kwa mgeni rasmi, walimu na wanafunzi wa madrasa hiyo wamesema wanakusudia kuanzisha skuli ya maandalizi ya kiislamu katika eneo hilo, lakini bado wanakabiliwa na tatizo la eneo la kujenga skuli hiyo.

Hivyo wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia eneo kwa ajili ya upanuzi wa madrasa yao pamoja na ujenzi wa skuli hiyo ya maandalizi.

Madrasat Azhar ilianzishwa mwaka 2011 ikiwa na wanafunzi 18, ambapo sasa imefikia idadi ya wanafunzi 100, wakiwemo wanawake 60 pamoja na walimu 7.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top