Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } unatarajia kutumia jumla ya shilingi za Kitanzania Bilioni 13.2 kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja kipya cha kufurahishia watoto cha ZSSF - UHURU unaoendelea hivi sasa kiliopo Kariakoo Mjini Zanzibar.

Ujenzi huo ulioanza mwezi Oktoba mwaka 2012 chini ya wataalamu wa Kampuni ya Ujenzi ya Kimataifa ya CRJE kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China unatarajiwa kukamilika Mwezi April mwaka huu.

Uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanja hicho cha ZSSF –UHURU ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 umefanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Kiwanja hicho cha kisasa kimezingatiwa uwekwaji wa pembea 10 mpya na nyengine kumi za Maji zilizotengenezwa Nchini china pamoja na maduka 57 mengi kati yake yakihudumia bidhaa za watoto.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanja hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi uamuzi wa ZSSF kuendeleza mradi huu umelenga kuweka mazingira mazuri kati ya wazazi na ambayo yataleta furaha na faraja kati ya pande hizo mbili.

Aliipongeza ZSSF kwa hatua iliofikia na akaitaka kutobweteka na miradi iliyoanzisha bali ni vyema ikatafuta maeneo mengine zaidi ya uwekezaji hususan katika vitega uchumi visivyohamishika na vyenye usalama zaidi.

Alisema hatua hiyo itasababisha ZSSF kuongeza rasilimali zaidi ambazo zitasaidia kuufanya Mfuko huu kuwa tegemeo kubwa kwa jamii na Serikali kuwa imara zaidi sambamba na kuuepushia Mfuko huo na janga la kufilisika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza uamuzi wa Waziri wa Fedha Zanzibar aliouchukuwa wa kukubali kusamehe ushuru wa kodi ya vifaa vya ujenzi wa Kiwanja hicho.

“ Tunastahiki tumshukuru Waziri wa Fedha pamoja kwamba jukumu lake ni kukusanya fedha zinazotokana na ushuru lakini leo ameamua kusamehe kodi ya ushuru wa vifaa vya ujenzi wa kiwanja hicho ili kazi ya ujenzi iende haraka kwa faida ya kuwapa fursa ya michezo watoto wa Taifa hili “. Alipongeza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea matarajio yake makubwa kutokana na eneo la kati kati ya Mji wa Zanzibar Michenzani na na Kariakoo litaendelea kubadilika la kuleta haiba nzuri kutokana na ujenzi wa majengo ya kiuchumi burdani pamoja na michezo.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Abdullwakil Haji Hafidh alisema mradi wa ujenzi wa kiwanja cya kufurahishia watoto cha ZSSF – UHURU mbali ya kutoa ajira kwa wafanyakazi wapatao mia moja lakini pia utaongeza tija za Kiuchumi.

Ndugu Abdullwakil alisema uwanja huo utakaokuwa na uwezo wa kuingiza mapato ya shilingi Bilioni 1.5 kila mwaka unatarajiwa kujilipa katika kipindi cha miaka kumi ijayo ukiwa na uwezo wa kuhudumia watu wasiopungua 15,000 kwa wakati mmoja.

Alifahamisha kwamba ndani ya uwanja huo itakuwemo michezo ya ndani { Video Games },jukwaa la maonyesho mbali mbali, Kahawa,jengo la utawala, mahitaji ya watu wenye ulemavu pamoja na vyoo 30.

Akimkaribisha Balozi Seif Waziri wa Fedha Zanzibar Mh. Omar Yussu Mzee alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesamehe ushuru zaidi ya shilingi Milioni mia tatu kutokana na uingizwaji wa vifa vya ujenzi vya kiwanja hicho hapa Nchini.

Waziri Yussuf aliuomba Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } kuzingatia viingilio itakavyoweka havitokuwa vikwazo kwa wananchi wenye kipato cha chini ili vilete faraja kwa wazazi hao na watoto wao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top