Uongozi wa Wizara ya Fedha ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania umekumbushwa kuzingatia uadilifu wakati unapotekeleza majukumu yake hasa yale masuala yanayohusu Zanzibar ikiwa ni njia moja wapo ya kuendelea kupunguza au kuondosha kabisa kero za Muungano.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Uongozi Mpya wa Wizara ya Fedha ya Serikali ya Muungano ukiongozwa na Waziri wake Mh. Saada Mkuya aliyefuatana na Manaibu wake wawili Mh.Adam Malima na Mh. Mwigulu Nchemba walipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi mara baada ya kuteuliwa kushika nyadhifa hizo.

Balozi Seif alisema licha ya juhudi na mafanikio makubwa yaliyochukuliwa na Viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali zote mbili chini ya Kamati ya pamoja ya kutatua kero za Muungano lakini bado juhudi za ziada zinapaswa kuchukuliwa ili kuona kero zilizobakia zinapatiwa ufumbuzi na kubakia kuwa historia tu hapa Nchini.

Alisisitiza kwamba huu ni wakati kwa Uongozi huo kuhakikisha kwamba yale mambo ambayo yanatakiwa kuchukuliwa hatua na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yanapaswa kufanywa kwa uadilifu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Waziri wa Fedha Mh. Saada Mkuya pamoja na Manaibu wake kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo akielezea matumaini yake kwamba watafanya kazi kwa ushirikiano pamoja na upendo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya ujumbe aliouongoza Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Saada Mkuya aliahidi kufanya operesheni maalum ya kuondoa kero za Muungano katika kipindi kifupi kijacho.

Mh. Saada alisema hilo litawezekana iwapo suala la mawasiliano litazingatiwa kuwa la msingi pamoja na kujenga nguvu za pamoja katika ushiriki wa vikao vya pande zote mbili vitakavyokuwa vikifuatilia utekelezaji wa mikakati inayowekwa na kukubalika.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo na ujumbe wa Wawekezaji wa Sekta tofauti ya kiuchumi kutoka Nchini Italy ambao upo Zanzibar kuangalia mazingira ya jinsi watakavyoweza kuwekeza vitega uchumi vyao.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar Kiongozi wa Ujumbe huo Rais wa Chama cha Mchezo wa Karati Duniani Profesa Martin Antonio Morina alisema ujumbe huo umevutiwa na mazingira mazuri yaliyopo ndani ya Visiwa vya Zanzibar jambo ambalo limewapa ushawishi wa kutaka kushirikiana na Zanzibar katika Sekta ya uwekezaji.

Profesa Martin Antonio alimueleza Balozi Seif kwamba ujumbe wake uko katika harakati za kuonana na Taasisi husika za uwekezaji hapa Zanzibar katika kuona wanaweza kuwekeza katika ujenzi wa Kituo cha Michezo { Sports Academy }, Huduma za Afya katika Sekta ya Utalii pamoja na suala la Umeme wa jua.

Alisema Wafadhili na wataalamu wa sekta hizo tatu tayari wameshaonyea niya ya kutaka kuanzia miradi hiyo ili isaidie kuinua sekta ya Utalii ambayo inaonekana kupewa msukumo mkubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na kutoa ajira kwa Wananchi wazalendo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza ujumbe wa wawekezaji hao kutoka Nchini Italy kwamba Zanzibar imeacha milango wazi kipindi kirefu sasa kwa kukaribisha wawekezaji wa Kigeni kusaidia miradi ya kiuchumi hapa Nchini.

Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na nia ya wawekezaji hao kutaka kuwekeza miradi yao ambayo kwa kiasi kikubwa ile waliyoipendekeza imekuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Zanzibar hasa katika kipindi hichi cha mabadiliko ya sayansi na Teknolojia Duniani.

“ Sekta zote mlizoainisha kutaka kuzitekeleza hapa Nchini ambazo ni Ujenzi wa Kituo cha Michezo, Hudumza za Umeme pamoja na huduma za afya katika Sekta ya Utalii ni muhimu “. Alisema Balozi Seif.

Ujumbe huo wawekezaji kutoka Nchini Italy umebeba wataalamu wa nawekezaji kutoka katika sekta za Michezo mbali mbali , Nishati, huduma za Afya pamoja na Utalii.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top