Wakati umefika kwa wasomi wanaomaliza masomo yao ya Vyuo Vikuu vya ndani na nje ya Nchini kuelekeza nguvu zao ubunifu wa ajira badala ya ile dhana ya kusubiri ajira kutoka Serikalini ili kuitumia vyema elimu waliyoipata vyuoni.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu KILIONI Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema wakati Serikali Kuu inaendelea na juhudi za kuimarisha Miundo mbinu ya Elimu Wasomi hao wanapaswa kujizatiti katika kuhakikisha wanapambana vilivyo na tatizo la ajira ambalo huonekana kuwakumba zaidi vijana wanaomaliza elimu yao.

Hata hivyo alisema Taifa pamoja na Wananchi wanaendelea kushuhudia kasi kubwa ya maendeleo ya Kiuchumi na ustawi wa Jamii katika Taasisi za Umma na hata zile za Kibinafsi inayotokana na mchango mkubwa unaotolewa na wasomi mbali mbali waliobahatika kupata taaluma ndani ya vyuo vikuu hivyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amelipongeza Shirika la maendeleo ya misaada la African Muslim Agency kwa misaada yake inayotoa katika sekta za maendeleo zaidi likilenga kwenye misaada ya Elimu zote ile ya Dini na Dunia.

Alisema Taasisi hiyo ya misaada ya maendeleo imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumkla kiasi kwamba ushirikiano huo unapaswa kuendelezwa zaidi.

Mapema Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Cukwani Profesa Hamed Rashid Hikman alisema Uongozi wa chuo hicho tayari umeshaongeza masomo mengine zaidi ili kukifanya chuo hicho kuwa na hadhi kamili ya chuo kikuu inayokubalika mahala popote ulimwenguni.

Dr. Hikman alifahamisha kwamba hatua hiyo ina lengo la kuwajengea mazingira mazuri wanafunzi wanaoamuwa kujipatia taaluma kwenye chuo Kikuu hicho cha Elimu.

Akitoa salamu zake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chukwani Dr. Abdulrahman El – Muhailan ameupongeza ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kuweit katika kuwajengea msingi bora wa kitaaluma vijana wa mwambao wa Afrika Mashariki.

Dr. Abdulrahman alisema ushirikiano huo umelipa shirika la maendeleo ya misaada la African Muslim Agency kusimamia vyema chuo hicho jambo ambalo limekiwezesha kuwa miongozi mwa vyuo vinavyokubalika vyema ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Jumla ya wanafunzi 265 wamefanikiwa kukamilisha mafunzo yao ya shahada ya kwanza ya mwaka 2011 hadi 2013 katika fani ya sayansi, sanaa pamoja na lugha za Kiswahili na Kiarabu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top