Waziri wa Kazi na Utumishi wa Umma wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Haroun Ali Suleiman aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili Kitengo cha mifupa { MOI } Mjini Dar es salaam kutokana na matatizo ya ugonjwa wa Moyo { Blood Pressure } Kesho Jumamosi Tarehe 17 Januari 2014 anasafirishwa kupelekwa Nchini Afrika ya Kusini kwa uchunguzi na Matibabu zaidi ya afya yake.

Hatua za mwisho za safari yake inayogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekamilika baada ya kurejea kwa unafuu wa afya yake iliyokuwa imetengemaa kwa takriban wiki moja sasa.
Waziri Haroun alipata matatizo ya maradhi ya moyo Ijumaa iliyopita na kupatiwa huduma za afya Zanzibar na kutokana na hali yake kutokuwa ya kuridhisha ikilazimika kusafirishwa kwa matibabu zaidi katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili Mjini Dr es salaam.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na wasaidizi wake alipata wasaa wa kufika Muhimbili kufutilia maendeleo ya afya ya Mtendaji wake Waziri Haroun.

Akimfariji Waziri huyo wa Kazi na Utumishi wa Umma Zanzibar Balozi Seif alimtakia afya njema na kupona haraka ili arejee nyumbani kuendelea kutekeleza majukumu aliyokabidhiwa na Taifa.

Balozi Seif alisema ukimya wa Waziri Haroun uliokuwepo katika kipindi hichi kifupi katika matukio mbali mbali ikiwemo Vikao vya Baraza la Mapinduzi umepunguza mchango wake uliozoeleka ambao hupenda kuutoa mara kwa mara.

Naya kwa upande wake Waziri wa Kazi na Utumishi wa Umma Zanzibar Mh. Haroun Ali Suleiman ameishukuru Serikali ya kwa mchango mkubwa iliyoutoa katika kushughulikia afya yake wakati wote alipokuwa Hospitalini hapo.

Waziri Haroun alielezea faraja yake kutokana na moyo ulioonyeshwa na Viongozi mbali mbali wa Kiserikali, Kisiasa wakiongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuamua kumtembelea kujua maendeleo ya afya yake.

Aliendelea kumuomba mwenyezi Muungu azidi kuwapa moyo wa huruma na upendo viongozi hao kuzidi kuwa karibu na wananchi wanaowaongoza katika sehemu mbali mbali nchini.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top