Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongezwa kwa hatua iliyochukuwa ya kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kwa mafanikio makubwa na ya kupigia mfano.

Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Marekani na Canada Balozi Liberata Mulamula wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Liberata Mula mula alisema maadhimisho hayo yaliyofikia nusu Karne yameijengea Historia kubwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika muelekeo wa maendeleo ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.

Alisema Mataifa mbali mbali duniani yameendelea kushuhudia hatua kubwa zilizofikiwa na Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo akiitaja baadhi yake imo katika sekta ya Afya, Maji, Mawasiliano ambayo tayari imeshajengewa miundo mbinu imara.

“ Huu ni mwaka wa Kihistoria kwa Zanzibar na Tanzania katika kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964. Sasa kinachowapaswa wananchi na viongozi wote kuhakikisha historia hii inaendelezwa zaidi katika misingi ile ile ya amani na utulivu “. Alisema Balozi Liberata Mula mula.

Balozi Mula mula alielezea kwamba katika muelekeo wa kujiandaa na sherehe za maadhimisho ya kutimia miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Uongozi wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani na Canada tayari uko mbioni kujiandaa na tamasha kubwa litakalolenga kutangaza maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania katika kipindi hicho.

Alisema Ofisi yake iko wazi na huru wakati wote kujumuisha pamoja na taasisi mbali mbali ziwe za Serikali au Binafsi katika kuchangia na hatimae kufanikisha Tamasha hilo muhimu katika kuitangaza Tanzania kiuwekezaji.

Akizungumzia kuhusu ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Mjini Seattle Nchini Marekani mwishoni mwa Mwaka jana Balozi Liberata Mula mula alisema yapo mafanikio makubwa yaliyojitokeza kufuatia ziara hiyo ambayo yanatarajiwa kuinufaisha kiuchumi Zanzibar.

Balozi Mula mula alisema kilichopo hivi sasa ni kuhakikisha taasisi zinazohusika na ziara hiyo kuendelea kufuatilia mazungumzo au makubaliano iliyofikia ili lengo la ziara hiyo liweze kufanikiwa vyema.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar ina mategemeo makubwa ya kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji katika sekta ya utalii kutokana na miundo mbinu mbali mbali iliyowekwa.

Balozi Seif aliuomba Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani na Canada kuhakikisha kwamba unaendelea kuitangaza Zanzibar kiuwekezaji ili washirika na taasisi za maendeleo wapate nafasi ya kuitumia fursa hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza watendaji wote wa Ofisi za Kibalozi za Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani kwa kufanya kazi za kizalendo licha ya kukabiliwa na mazingira magumu ya kikazi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top