Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amefika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwajuilia hali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma mhe. Haroun Alim Suliman, pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Cleopa David Msuya waliolazwa katika hospitali hiyo.

Wawili hao wamelazwa katika hospitali hiyo wakisumbuliwa na matatizo ya moyo.

Wakizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais, wamesema wanaendelea vizuri na kwamba afya zao zinaendelea kuimarika siku hadi siku, tofauti na walipofikishwa hospitalini hapo.

Waziri Haroun anatarajiwa kupelekwa nchi Afrika ya Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewaombea viongozi hao wapone haraka ili waendelee na majukumu ya kulitumikia taifa.

Wakati huo huo Maalim Seif ameshiriki katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu George Bakari Liundi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa na vyama vya siasa wakiwemo Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Mohd Gharib Bilal.

Marehemu Geoge Liundi ambaye alikuwa msajili wa kwanza wa vyama vingi vya siasa nchini kuanzia mwaka 1992 hadi 2004, alifariki jijini Dar es Salaam tarehe 12 januari, 2014 kutokana na shinikizo la damu.

Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge Mhe. Willium Lukuvi, amesema marehemu alikuwa mtumishi wa muda mrefu katika serikali, na atakumbukwa kutokana na mchango wake ndani na nje ya serikali.

Amesema miongoni mwa mambo ya msingi yanayoacha kumbukumbu nzuri kwa marehemu George Liundi, ni pamoja na kuweka misingi imara ya sheria akiwa mwandishi mkuu wa kwanza wa sheria, pamoja na msajili wa kwanza wa vyama vya siasa.

Mapema akisoma wasifu wa marehemu, mwakilishi wa familia hiyo amesema marehemu George Liundi alizaliwa mwaka 1938 katika Wilaya ya Masasi na amewahi kushika nyadhifa mbali mbali za serikali ikiwa ni pamoja na uwakili, Naibu Mwanasheria Mkuu na balozi nchini Switzerland.

Amesema familia imepoteza mtu makini, imara na muadilifu ambaye ametoa mchango mkubwa katika familia na taifa kwa ujumla.

Salamu za vyama vya siasa zikiwasilishwa na Emannuel Makaidi zimesema kuwa marehemu George Liundi alikua mtu makini na asiyetabirika katika utendaji wake, na kwamba taifa limepoteza mtu muhimu katika ulingo wa siasa.

Amesema George Liundi ni kiongozi wa kuigwa kutokana na uwelewa aliokuwa nao wa kujioni mtu wa kawaida licha ya kuwa ni kiongozi mkubwa na hakupenda kujitajirisha.

“Marehemu huyu alikuwa mtu mkubwa lakini akijifanya mtu wa kawaida, ameondoka duniani hakuacha maghorofa wala mabangaloo, ni mtu wa kuigwa sana katika jamii yetu”, alisisitiza Makaidi.

Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top