Jeshi la Polisi nchini limesema litaendelea kushirikiana na raia katika jitihada zake za kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, wakati akizungumza na Makamu wa Kanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ofisini kwake Migombani.

IGP Mangu ambaye aliambatana na Naibu wake Abrahmani Kaniki pamoja na kamishna wa polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame, amesema suala la kudhibiti uhalifu ndio jukumu la msingi la jeshi la polisi, na kwamba litafanyiwa kila juhudi kuona kuwa vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa.

Ameongeza kuwa jeshi la polisi kamwe halipendi kuona kuwa linakuwa chanzo cha vurugu, bali kuzuia vurugu pale zinapotokea na kurejesha amani pale inapotoweka.

Aidha IGP Mangu amesema jeshi hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika jitihada zake za kukuza uchumi na kupunguza umaskini, kwa kutunza usalama katika maeneo ya utalii ambao ndio sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar.

Amefahamisha kuwa suala la amani na usalama ni jambo la msingi katika nchi, na kwamba hali hiyo ndio msingi mkuu wa kuvutia wawekezaji wa sekta mbali mbali hasa utalii.

Hivyo amesema wataweka mkazo katika maeneo ya utalii ili kuhakikisha kuwa hakuna vitisho wala madhara yanayopatikana kwa wageni wanaoingia nchini.

IGP Mangu amesema ingawa jeshi hilo bado linakabiliwa na upungufu wa vitendea kazi vya kisasa, lakini watatumia rasilimali zilizopo katika kuimarisha utendaji wake.

Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema suala la ulinzi wa raia na mali zao linapaswa kupewa kipaumbele cha mwanzo katika utendaji wa jeshi hilo.

Amesema amani na usalama ndio chachu ya maendeleo kwa uchumi wa Zanzibar ambayo inategemea zaidi sekta ya utalii.

Amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi aliyepita IGP mstaafu Said Mwema, kwa wazo lake la kuanzisha polisi jamii ambayo imeliweka karibu zaidi jeshi hilo na wananchi.

Amemtaka IGP Mangu kuliendeleza wazo hilo, kwani linasaidia kuondosha khofu kwa raia dhidi ya polisi.

Amesisitiza haja kwa jeshi la polisi kuendeleza mahusiano mema na raia, ili kuwawezesha wananchi kujenga imani na jeshi hilo, hatua ambayo itasaidia utendaji wa jeshi.

Aidha Maalim Seif amewataka watendaji wa jeshi la polisi kutunza siri za watu wanaowapelekea taarifa zikiwemo za uhalifu, ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Sambamba na hilo amelikumbusha jeshi hilo kuwadhibiti watuhumiwa wa uhalifu pale wanapopewa taarifa na kuwakamata, ili kuepusha dhana kuwa jeshi hilo linalea wahalifu.

“Wakati mwengine anaweza kukamatwa mtuhumiwa sugu wa uhahifu kwa msaada wa raia wema, lakini baada ya siku mbili au tatu mtuhumiwa huyo anaonekana kudunda mitaani. Jambo hili linaondoa imani kwa raia hao dhidi ya polisi”, alitanabahisha Maalim Seif.

Katika hatua nyengine Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amempa changamoto IGP Mangu ya kulisafisha jeshi hilo dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyodaiwa kuliandama jeshi hilo.

Amesema katika kulisafisha jeshi hilo dhidi ya vitendo vya rushwa, hakuna budi kwa viongozi kuondosha muhali wakati wanapoamua kuwashughulikia watendaji wanaoendesha vitendo hivyo.

“Tunataka jeshi letu liwe safi kwa kuwashughulikia watendaji wanaojihusisha na rushwa, na katika hili ni lazima muondoshe muhali”, alisisitiza Maalim Seif.

Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top