Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi ameiasa Jamii kwamba uigaji wa hulka na Tabia za kigeni zinazoonekana kulikumba zaidi kundi kubwa la Vijana unazalisha malezi mabovu yanayokwenda kinyume na Utamaduni wa Taifa  hili.

Kauli hiyo aliitowa kwenye halfa ya mahafali ya wazazi pamoja na maadhimisho ya kutimia miaka mitano ya Philter Federal School iliyopo Fuoni Meli Tano nje kidogo ya Mji wa Zanzibar zilizofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

Mama Asha alisema wakati dunia inaendelea kupitiwa na mabadiliko makubwa ya mitandao ya Teknolojia wazazi wanapaswa kuwa makini kipindi hichi cha mpito katika kufuatilia nyendo za watoto wao.

Alisema licha ya muda mwingi wa watoto hao unakuwa ndani ya himaya ya walimu lakini bado Wazazi wanawajibu mkubwa wakuhakikisha wanashirikiana na walimu hao katika kuwafinyanga watoto wao kuelekea katika njia sahihi.

Katika kuimarisha kiwango cha elimu maskulini hasa kwa zile skuli za binafsi zinazojitegemea zenyewe Mama Asha alisema wazazi wahakikishe wanalipa ada za watoto wao kwa wakati ili kutoa nafasi kwa walimu kuendelea kusomesha kwa utulivu.

Aliupongeza Uongozi wa Philter Federal School kwa juhudi unaochukuwa wawafinyanga watoto wao na kuwa mahiri kimasomo na hata ushiriki wao wa michezo mbali mbali.

Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuahidi Uongozi wa Skuli hiyo kwamba atakuwa tayari kusaidia nguvu za skuli hiyo katika kuona lile lengo walilojipangia la kutoa elimu bora na safi linafanikiwa vyema.

Akisoma Risala ya Skuli hiyo Mwanafunzi Hassan Hassan Lukoma alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya skuli hiyo katika kipindi cha miaka mitano tokea ilipoanzishwa mwaka 2009.

Mwanafunzi Hassan alisema Philter Federal School imekuwa ikiendelea kutoa wanafunzi mbali mbali wa michepuo kuingia kiwango cha sekondari katika masomo ya sanaa, Sayansi pamoja na biashara.

Alisema katika kuimarisha ufaulu wa wanafunzi wa Skuli hiyo juhudi zimechukuwa na uongozi wa skuli hiyo katika kujiandaa na ufundishaji wa Lugha za kigeni zitakazotoa furtsa na wigo wa kuimarika kwa kiuchumi kutokana na kukomaa kwa kiwango cha elimu Kimataifa.

Hata hivyo mwanafunzi Hassan Hassan alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili skuli hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa vifaa vya sayansi, uhaba wa vikalio pamoja maslahi duni ya walimu kutokana na wazazi kuchelewa kulipa ada za watoto wao.

Mapema Mkurugenzi Utumishi Wizara ya Elimu an maafunzo ya Amali Zanzibar Nd. Vuai Khamis Juma alisema katika kusaidiana na Skuli Binafsi Wizara ya Elimu imeandaa utaratibu maalum wa kugawa vitabu ilivyonavyo kwa kuzipatia skuli binafsi.

Nd. Vuai alitoa wito kwa walimu wa skuli hiyo kusomesha kwa bidii na uadilifu na kuwaomba wanafunzi wao kuepuka tabia ya kughushi mitihali yao jambo ambalo litachangia kuviza kiwango cha elimu pamoja na upatikanaji wa wataalamu waliobobea.

Katika hafla hiyo iliyoshuhudiwa na wazazi kadhaa wa wanafunzi Mama Asha alikabidhi vyeti kwa wanafunzi wa Skuli ya Maandalizi na wale wa Darasa la kumi na mbili { Form IV } waliomaliza masomo yao.

Pia hafla hiyo ilijumuisha michezo mbali mbali iliyochezwa na wanafunzi hao wa maandilizi na Sekondari wakionyesha umahiri wao uliotoa burdani safi katika viunga vya Hoteli ya Bwawani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top