Uwamuzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } Kikosi cha 14 cha Ali Khamis kiliopo Vitongoji Chake chake Kisiwani Pemba wa kuanzisha Skuli ya Maandalizi, Msingi na hatimae muelekeo wa Sekondari umesaidia kuunga mkono azma ya Serikali kupitia Sera ya Elimu ya kulenga kuwapatia Elimu ya lazima watoto wote wa Taifa hili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Jengo Jipya la Skuli ya Maandalizi ya Ali Khamis Camp iliyoanzishwa na Makamanda na wapiganaji wa Kikosi hicho cha 14 Vitongoji hafla ambayo ilipata baraka pia na wazazi na wanafunzi wa Skuli hiyo.

Balozi Seif alisema jamii inafahamu juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } katika kusaidia masuala ya Kijamii katika wakati wa amani jambo ambao huleta faraja kwa wananchi wanaozizunguuka kambi za Jeshi hilo katika maeneo mbali mbali Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikipongeza Kikosi hicho cha 14 cha Ali Khamis kiliopo Vitongoji Chake Chake Pemba chini ya usimamizi wa Mkuu wa Kikosi hicho ambae ndie muanzilishi wa Skuli Hiyo Luteni Kanali Julius Khombwe Mbwelo kwa wazo lao la kufikiria kuanzisha skuli hiyo.

Balozi Seif alisema uwamuzi huo umekuja katika kipindi muwafaka utakaochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye skuli za Serikali zinazozizunguuka Kambi hiyo.

Alielezea faraja na kuvutiwa na uamuzi wa kizalendo wa Jeshi hilo wa kukubali kuwapokea watoto wa raia wa jirani na Kambi hiyo ambao ni wa kupigiwa mfano na Serikali Kuu inaangalia mazingira ya kuisaidia Skuli hiyo ambayo kwa mazingira yake inahesabika kama ni skuli ya umma licha ya kwamba inahudumiwa kwa nguvu za wanajeshi wenyewe.

“ JWTZ linafahamika kwa kuanzisha miradi mbali mbali inayosaidia jamii katika maeneo tofauti Nchini ikiwemo Skuli za msingi na Sekondari, Vituo vya Afya na hata kazi za kujitolea “. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma kwenye skuli hiyo kuhakikisha kwamba wanatoa ada zao ndogo walizopangiwa kwa wakati ili huduma za wanafunzi zinazotolewa skulini hapo ziendelee kama kawaida.

Katika kuunga mkono juhudi za Makambanda na wapiganaji wakambi hiyo ya 14 Vitongoji Chake Chake Pemba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliahidi kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar katika kuhakikisha Skuli hiyo inaondokana na tatizo la huduma za Umeme.

Balozi Seif pia aliahidi kuchangia gharama za matofali elfu moja yatakayosaidia kuendeleza ujenzi wa jengo aliloliwekea jiwe la nsingi la Skuli ya Maandalizi pamoja na kusaidia mipira kumi ya mchezo wa soka na kumi ya mchezo wa Pete.

Akitoa Taarifa fupi ya Skuli ya Kikosi cha 14 cha Ali Khamis Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo mwalimu Yugin Lutagengwa alisema skuli hiyo ilianzishwa mwaka 2009 ikiwa na wanafunzi 39 na sasa wamefikia 604 wengi wao wakia raia wa jirani wanayoizunguuka skuli hiyo.

Mwalimu Yugin Lutagengwa alisema lengo la kuanzishwa kwa skuli hiyo chini ya Mkuu wa Kikosi hicho Luteni Kanali Juius Khombwe Mbwelo ni kushiriki kwa wanajensi katika Jamii wakati wa amani pamoja na kupunguza maafa kwa watoto hasa pale wanapofuata elimu masafa ya mbali.

Hata hivyo Mwalimu Mkuu Yugin alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili skuli hiyo kuwa ni pamoja na jamii kutoelewa elimu ya ushindani, uhaba wa majengo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi pamoja na tatizo la huduma za umeme.

Katika Risala yao iliyosomwa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Skuli hiyo Mwanafunzi Ridhiwan Khalfan Hamad wameelezea kufarajika kwa kiwango cha elimu wanachokipata katika skuli yao.
Hata hivyo wanafunzi hao waliiomba Serikali na wafadhili kufikiria wazo la kuwapatia huduma za mitandao Kompyuta ambayo wanaimani kwamba itaongeza nguvu zao za ufahamu katika masomo yao mbali mbali.

Mapema Kamanda wa Kikoci cha 14 cha Ali Khamis kiliopo Vitongoji Chake chake Pemba Luteni Kanali Julius Khombwe Mbwelo alisema katika kuwajengea mazingira bora ya kufaulu vyema wanafunzi wao Uongozi wa Skuli hiyo uko katika juhudi za kujenga Bwalo la wanafunzi ili kuwapa utulivu katika masomo yao.

Kamanda Julius alisema hatua hiyo imelenga kuwaanda vizuri wanafunzi wa darasa la saba walioingia mwaka huu ambao wanatarajiwa kufanya mtihani wa Taifa kwa ajili ya kujiwekea malengo ya kuingia skuli za Sekondari za Mchepuo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikagua Hospitali ya Jeshi hilo iliyopo jirani na eneo hilo ambayo pia hutoa huduma za afya kwa askari pamoja na wananchi wanaolizunguuka eneo hilo.

Hospitali hiyo kubwa imefanyiwa matengenezo makubwa kwa msaada wa Serikali ya marekani ambapo baadaye inatarajiwa kuongeza huduma zake za afya likiwemo suala la kulaza wagonjwa.

Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Kepteni Said Omar Mwege alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif change moto wanazokabiliana nazo kubwa likiwa ongezeko la wagonjwa ambapo uwezo wa kuwapatia huduma za dawa ni mdogo.

Kepteni Said alieleza kwamba licha ya mashirikiano mazuri yaliyopo kati ya Uongozi wa Kambi hiyo na Uongozi wa Wizara ya Afya Pemba lakini suala la upatikanaji wa dawa Hospitalini hapo linahitaji kuungwa mkono ya Serikali.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliueleza uongozi wa Hospitali hiyo kwamba Serikali itaangalia nama ya kuiwezesha Hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi.

Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Hospitali hiyo kupitia Mkuu wa Kambi hiyo kuorodhesha mapungufu yote yaliyomo ndani ya Hospitali hiyo ikiwemo wafanyakazi ili Serikali ijipange katika kuona inatoa msukumo kwa Hospitali hiyo.

Aliopungeza Uongizo wa Kambi hiyo katika juhudi za kuimarisha huduma za afya kwa uwamuzi wake wa Kujenga jengo jipya la huduma za uchunguzi wa X Ray,Utra sound pamoja na ushauri nasaha kwa wananchi walioambukizwa na virusi vya Ukimwi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi aliueleza Uongozi wa Hospitali hiyo kwamba yeye binafsi ataangalia mazingira ya kusaidia vitanda vya wagonjwa kwa ajili ya Hospitali hiyo katika kipindi kifupi kijacho.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top