Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake kitaendelea kusimamia misingi ya haki na usawa, ili kuhakikisha kuwa kila Mzanzibari anapata haki yake inayostahiki.

Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara ya chama hicho uliofanyika viwanja vya Kinyasini, jimbo la Chaani.

Amesema Chama hicho kiko mstari wa mbele kudai mamlaka kamili ya Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha kuwa Zanzibar inaongozwa na wazanzibari wenyewe bila ya kuingiwa na mamlaka nyengine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maridhiano mzee Hassan Nassor Moyo, amebainisha kuwa mambo yanayodaiwa kutolewa katika Muungano sio mageni, kwani yalikuwemo kwenye mamlaka ya Zanzibar kabla ya kuungana na Tanganyika mwaka 1964.

Amewasisitiza Wazanzibari kuepukana na chuki, fitna na ubaguzi, na badala yake waungane kupigania maslahi ya nchi yao.

Nae Mjumbe wa Kamati hiyo ya maridhiano Mansoor Yussuf Himid, amesema Zanzibar ni ya Wazanzibari wote, na kwamba kila mzanzibari anastahili kupata haki sawa na mwengine.

Amesema ataendelea kuungana na Wazanzibari kupigania haki ya Zanzibar ndani ya Muungano, ili iweze kuendesha mambo yake yenyewe.

Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top