Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amempongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza kwa juhudi anazoendelea kuchukuwa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2010 sambamba na ahadi alizotowa wakati alipoomba ridhaa kwa wananchi kuongoza Jimbo hilo.

Alisema Mwakilishi huyo ametimiza agizo la Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mojd Sheni alilolitoa la kutaka wana CCM na Viongozi wao kushirikiana katika kuzifufua tena Maskani za Chama cha Mapinduzi katika maeneo mbali mbali Nchini.

Balozi Seif alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kuizindua Maskani Mpya ya Wazee wa CCM iliyopo katika Kijiji cha Ndagaa ndani ya Jimbo la Uzini ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kusherehekea Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alisema maskani ndizo chimbuko na uhai mkubwa wa Chama cha Mapinduzi kutokana na kundi kubwa la Wanachama wake kuwa washirika wakuu wa maskani mbali mbali hapa Nchini.

“ Nastahiki kumpongeza Mh. Mwakilishi wenu wa Jimbo hili la Uzini kwa umahiri wake wa kuiremba Maskani hii ya Wazee wa CCM Ndagaa akithamini mchango wenu mkubwa wa kupigania uhuru wa Nchi hii na kupatikana Mapinduzi Matukufu ya Mwaka 1964 yaliyoondoa dhulma na udhalilishaji ”. Alisema Balozi Seif.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaagiza Viongozi na Wanachama wa Chama hicho kuimarisha miradi mbali mbali itakayokisaidia chama kuendesha shughuli zake za kila siku.

Alieleza kwamba Chama cha Mapinduzi wakati wote kimekuwa kikisisitiza na kuagiza umuhimu wa wanachama wake kubuni na hatimae kuanzisha miradi itakayoibuwa mitaji ya kiuchumi ambayo ndio njia pekee itayokisaidia Chama kuondokana na tabia ya kutegemea ruzuku.

Mapema akisoma Taarifa fupi ya Maskani hiyo ya Wazee wa CCM Ndagaa Mjumbe wa Kamati ya Maskani hiyo Nd. Andrik Chumvi Mohd alisema maskani hiyo iliyoasisiwa mwaka 1993 ilianza na nyasi ikiwa na wanachama 33.

Ndugu Chumvi alisema Wanachama na Viongozi wa Maskani hiyo hivi sasa wamefarajia na ujenzi mpya wa maskani hiyo inayokwenda samba mba na hadhi ya chama cha Mapinduzi.

Hata hivyo Nd. Andri Chumvi alisema bado zipo changamoto na mapungufu yanayoikabili maskani na wanachama wake ikiwa ni pamoja na ukosefu wa Seti ya TV, Vifaa vya Ofisi pamoja na kuungwa mkono katika harakati zao za kuanzisha Kikundi cha Saccos cha Maskani hiyo.

Wakati huo huo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif alikabidhi Baskeli 48 kwa ajili ya kusaidia usafiri Viongozi wa Jimbo la Uzini kuweza kufuatilia kwa umakini majukumu waliyopangiwa.

Baskeli hizo zilizotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza zimekabidhiwa kwa Wenyeviti na Makatibu wa Matawi 19 yaliyomo ndani ya jimbo la Uzini, Wenyeviti na Makatibu wa Wadi tatu, Mwenyekiti na Katibu wa Jimbo hilo pamoja na Mratibu wa Maskani wa Wilaya ya Kati Ndugu Abdulla Maro.

Shughuli hiyo ilikwenda sambamba na Balozi Seif kukabidhi Track Suits 25 za kwa ajili ya Kikundi cha Mazoezi cha Wanawake cha Uzini { Upendo Exercise Group } pamoja na Viatu kwa ajili ya waamuzi watakaoendesha Mashindano ya michezo ya Kombaini ya Maskuli ya Wilaya za Zanzibar.

Akizungumza na Wenyeviti, Makatibu na Wanachama wa CCM wa Jimbo hilo Balozi Seif alisema kazi ya CCM katika kutafuta ushindi kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015 unaweza kuwa mgumu endapo viongozi na wana CCM wataendeleza tabia ya kuvutana.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba umefika wakati kwa Viongozi na Wanachama wa chama hicho kuziepuka tabia za baadhi ya viongozi wanaoshabikia na kuendeleza makundi ndani ya chama kwa maslahi yao binafsi.

Alisisitiza kwamba Viongozi katika kipindi hichi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao wanapaswa kusimamia vyema vikao vya Chama ambavyo kwa kiasi kikubwa mbali ya kutekeleza kanuni ya Chama lakini pia vinasaidia kupunguza majungu na fitina miongoni mwa Viongozi na wanachama wao.

Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza alipendekeza kwa Uongozi wa juu wa CCM Afisi Kuu chini ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar kuandaa utaratibu wa vikao vya kuwahoji Wabunge na Wawakilishi jinsi wanavyowajibika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mh. Raza alisema upo utaratibu mzuri ndani ya Mfumo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar { Maarufu Bango Kitita } unaotoa nafasi kwa Viongozi wa Mawizara ya Serikali kutakiwa kufafanua utekelezaji wa malengo waliyojipangia ya Mawizara yao katika kipindi cha kila baada ya robo mwaka.

Akitoa salamu zake kwenye hafla hiyo ya makabidhiano ya vipando vya usafiri kwa Wenyeviti na Makatibu wa Matawi, wadi na Jimbo la Uzini Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mama Asha Suleiman Iddi alikemea tabia ya makundi yanayoonekana kupaliliwa na baadhi ya Viongozi wa Matawi hayo.

Mama Asha alisema tabia hiyo mbaya mbali ya kudhoofisha nguvu za chama katika utekelezaji wa majukumu yake lakini pia inaongeza chuki na uhasama baina ya viongozi na wanachama wenyewe.

Msaada huo wa Baskeli uliotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza Hassan ambao ni utekelezaji wa ahadi aliyoitowa wakati wa kuomba ridhaa kwa wananchi wa jimbo hilo pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 umegharimu jumla ya shilingi Milioni 10,000,000/-.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

0 comments:

 
Top