Zanzibar imezindua safari za ndege moja kwa moja kutoka Johannesburg Afrika ya Kusini hadi Zanzibar.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika hoteli ya LAGEMA Nungwi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amelipongeza shirika la ndege la MANGO kutoka nchini humo kwa kuamua kuanzisha safari hizo.

Amesema safari hizo zitasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka Afrika ya Kusini, hasa ikizingatiwa kuwa watalii wa nchi hiyo tayari wameruhusiwa kuingia nchini bila ya kuwa na viza.

Amefahamisha kuwa Zanzibar inategemea sana sekta ya utalii katika kukuza uchumi wake, na kwamba kwa sasa ndio sekta kiongozi inayochangia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa asilimia 72.

Amesema serikali kwa upande wake itafanya kila juhudi kushirikiana na shirika hilo pamoja na wawekezaji wengine, ili kuhakikisha kuwa sekta ya utalii na uwekezaji zinapata maendeleo makubwa.

Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka watembezaji watalii pamoja na vyombo vya habari kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Zanzibar kwa wageni, ili kuvutia watalii na wawekezaji wengi zaidi.

Ameongeza kuwa lengo la serikali ni kuona kuwa inafanya kazi kwa karibu zaidi na wenzao wa Afrika ya Kusini katika sekta zote za maendeleo, ili kunyanyua hali za maisha kwa wananchi wa pande hizo mbili.

Kwa upande wake Balozi wa Afrika ya Kusini nchini Tanzania Bw. Thamduycse Chilliza amesema wananchi wa Afrika ya Kusini mara zote wamekuwa wakijisifia ukarimu wanaoupata kutoka kwa ndugu zao wa Tanzania, na kwamba hali hiyo imekuwa ikiwavutia wawekezaji wengi kutoka nchi hiyo.

Amesema uzinduzi wa safari hizo za moja kwa moja utarahisisha safari za watalii na wawekezaji wengine, sambamba na kukuza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hiyo na Zanzibar.

Amesema Tanzania imeendelea kuwa nchi muhimu barani Afrika kutokana na uwepo wa amani na usalama, tofauti na ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika, hali inayoipa nafasi kubwa zaidi ya kuvutia wawekezaji kutoka nchi mbali mbali duniani.

Nae Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Afrika ya Kusini katika kuimarisha vitega uchumi vyake Zanzibar.

Amesema hatua hiyo inadhihirisha ukweli kuwa Zanzibar ni mahali pazuri na salama kwa uwekezaji na wageni, na kulitakia shirika hilo la ndege mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma za usafiri wa ndege nchini.

Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top