1.MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaowakilishwa na zaidi ya mashirika 50 ya haki za binadamu hapa nchini kwa kushirikiana na Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Umoja wa Vilabu Vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa pamoja tumepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa juu ya hatua ya Serikali ya kufungia magazeti mengine mawili nchini – MWANANCHI na MTANZANIA.
Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kwa siku kumi na nne (14), huku gazeti la MTANZANIA likifungiwa kwa muda wa siku tisini (90).
Hatua hii ya serikali inafanya idadi ya magazeti yaliyofungiwa kufikia matatu. Julai mwaka jana serikali ililifungia gazeti la MwanaHALISI kwa muda usiojulikana.
Baada ya kutafakari kwa makini hatua hiyo, tunalaani vikali hatua ya Serikali kuendeleza tabia ya kibabe ya kuvitisha na kuvifungia vyombo vya habari nchini.
Hivyo basi, taasisi hizi kwa umoja wake, zimeona kufungiwa kwa magazeti haya ya wananchi kunaoyesha dhahiri nia ya serikali kutisha wananchi, kuleta hofu kwenye jamii na kuwanyamazisha wapigania haki za binadamu, vyombo vya habari, na watetezi wa haki za binadamu nchini.
Ni wazi kwamba hatua hii ya serikali ni ukiukwaji mkubwa wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 18 (1) (2) Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010.
2.Aidha, Serikali imeendelea kuitumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 (The Newspaper Act of 1976 Cap. 229, R.E. 2002) na Sheria ya Usalama wa Taifa (National Security Act of 1970, Cap. 47 [R.E 2002) kuvunja uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari nchini.
Sheria hizi kwa miaka mingi zimekuwa zikipigiwa kelele kwa kuwa ni sheria kandamizi; zinapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria za kimataifa.
Sheria hizo mbili zinampa mamlaka waziri anayesimamia habari kufungia gazeti au chombo chochote cha habari pale anapoona inafaa kufanya hivyo.
Sheria inamgeuza waziri kufanya kazi za uhariri, kushutumu, kushtaki, kuhukumu na kutekeleza hukumu. Hii ni kinyume na utawala wa sheria na kanuni za haki asili.
Katika tukio hili, misingi ya kanuni ya haki asili kama vile haki ya kusikilizwa na haki ya kukata rufaa mbele ya chombo kisichokuwa na maslahi yoyote katika shauri husika imevunjwa.
Kwa kuwa serikali ndiyo mlalamikaji haikupaswa kuachiwa tena kuwa mwendesha mashtaka na mtoa maamuzi katika suala hili.
Kufungiwa kwa magazeti haya huondoa haki ya kupata habari kama inavyotolewa na Ibara ya 19 ya Mkataba wa Haki za Kijamii na Kisiasa wa mwaka 1966 (ICCPR), Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu 1981. Kifungu cha 18 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 kinatoa uhuru wa maoni bila kikwazo cha aina yoyote.
Kwa kitendo hiki, Watanzania wengi wamenyimwa haki ya kupata taarifa na hivyo kupunguza uwajibikaji wa viongozi wa Serikali.
Aidha, hatua hii ya serikali inawanyima haki ya ajira waandishi wa magazeti hayo, wafanyakazi, wasambazaji na familia zao.
Mtandao wa Watetezi pamoja na wadau wengine tunawaomba Watanzania wote wenye mapenzi mema tushirikiane kufanya yafuatayo:
Kwanza, Serikali kufuta au kuzifanyia marekebisho sheria zote kandamizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza kama inavyopendekezwa mara kadhaa na wadau wa tasnia ya habari nchini.
Pili, kuyafungulia mara moja magazeti yote yaliyofungiwa ili kuwapa Watanzania taarifa na ajira.
Tatu, Serikali itumie njia shirikishi kama vile kutumia mahakama, MCT katika kupeleka malalamiko yake dhidi ya vyombo vya habari badala ya kuvifungia.
Nne, kwa kuwa katiba ndiyo sheria mama, Serikali iheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
3
Tano, vyombo vya habari kuvunja ukimya na kuonesha umoja wao katika suala hili, kwani kuumia kwa mmoja ni kuumia kwa wote.
Sita, vyombo vya habari kuendelea kutafuta na kutoa taarifa zote zenye tija na maslahi kwa umma.
Saba, asasi za kiraia na taasisi za habari kuongeza nguvu katika kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd dhidi ya Serikali kutaka kufutwa kwa Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.
Nane, tunaziomba Jumuiya za Kimataifa (UN) mawakala wake, balozi mbali mbali nchini na asasi zote za kikanda na za kimataifa wachukue hatua katika suala hili na matukio mengine yanayowaandama watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari nchini.
Tisa, tunaomba ieleweke kuwa taasisi za kidini, watetezi wa haki za binadamu, wanahabari na asasi za kiraia lengo ni moja la kufuatilia utendaji wa serikali. Hivyo basi, kufungiwa kwa moja kati ya hao ni tishio na ni kinyume na misingi ya haki za binadamu. Hivyo tunawaomba kwa umoja wao waitake Serikali kuyafungulia magazeti yote yaliyofungiwa mara moja.
Kwa kuwa umma ndiyo watu wa kwanza kupokea taarifa za vyombo vya habari, tunawaomba kuungana nasi pamoja na wadau wengine kupinga tukio hili.
Hili tamko la pamoja lilitolewa na kusainiwa leo, 30 Septemba 2013 na wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu na Wadau mbali mbali waliorodheshwa katika tamko hili.
0 comments:
Post a Comment