Wakati Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 68 tangu kuasisiwa kwake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeelezea kuridhishwa na jitihada za Umoja huo katika kuiunga mkono Zanzibar kupitia nyanja tofauti zikiwemo kuwajengea uwezo vijana pamoja na elimu ya afya hasa kwa akinamama na watoto.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo katika hafla maalum ya kuadhimisha siku siku ya Umoja wa Mataifa iliyofanyika hoteli ya Serena Mjini Zanzibar.

Amesema Umoja wa Mataifa umekuwa mstari mbele kuchangia juhudi za maendeleo nchini kupitia mashirika yake yakiwemo Shirika la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Shirika la kuhudumia watoto (UNICEF), Shirika la Kazi (ILO) na Shirika la Afya duniani (WHO).

Amesema mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na kuwepo kwa mashirika ya Umoja huo, na kwamba Serikali inathamini mchango wa Umoja wa Mataifa katika maendeleo ya nchi.

Amehamisha kuwa Serikali itaendeleza uhusiano mwema uliopo kati yake na Umoja wa Mataifa, na kuahidi kufanya juhudi za makusudi kuona kuwa malengo ya millennium yaliyoanzishwa na Umoja huo yanafikiwa ifikapo mwaka 2015.

Amesema pamoja na mambo mengine Umoja wa Mataifa umekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza umoja na mshikamano duniani, sambamba na kusimamia masuala ya amani, utawala bora na haki za binadamu.

Maalim Seif ametaja baadhi ya michango muhimu iliyotolewa na Umoja huo kwa Zanzibar kuwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za vijana hasa wa vijijini katika kukabiliana na tatizo la ajira, kusaidia mpango mkakati wa vijana Zanzibar, elimu, pamoja kusaidia juhudi za serikali katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Hata hivyo ameuomba Umoja huo kuongeza misaada yake kwa Zanzibar, hasa katika kuwawezesha vijana kuweza kukabiliana na ukosefu wa ajira na kupunguza umaskini.

Nae Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Alberic Kacou amesema wanaadhimisha siku hiyo kutathmini hatua zilizofikiwa na Umoja huo katika kutunza amani na maendeleo duniani.

Amesema katika tathmini yake kwa mwaka 2013, Umoja huo unakabiliwa na changamoto ya kiusalama kutokana na mapigano yanayoendelea nchini Syria.

Amesema mamilioni ya watu wamekuwa wakiutegemea Umoja huo kwa misaada ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na janga la njaa, na kwamba hautosita kutoa misaada hiyo kwa kadri itavyohijatika katika nchi mbali mbali.

Kuhusu malengo ya millennium, Kacou amezitaka nchi wanachama kuendeleza juhudi ili kuona kuwa zinafikia malengo hayo ifikapo mwaka 2015, huku akilenga zaidi suala la kupunguza umaskini.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na vingozi mbali mbali wakiwemo mabalozi wadogo waliopo Zanzibar, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Abdulhamid Yahya Mzee.

Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top