Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewahimiza Masheha Nchini kuhakikisha kwamba sheria na taratibu zilizowekwa katika zoezi la uandikishaji wa Wananchi kwenye Daftari la Kudumu la wapiga kura zinafuatwa kikamilifu.

Alisema hatua hiyo ndio njia pekee itakayowezesha kila mwananchi aliyefikia umri au kukamilisha taratibu za kujiandikisha anapata haki hiyo bila ya kunyanyaswa kwa sababu tu ya itikadi za kisiasa.

Balozi Seif alitoa himizo hilo wakati akizungumza na Masheha wa Wilaya ya Mkoani na baadhi ya Masheha wa Wilaya ya Chake chake mkoa wa Kusini Pemba katika Ukumbi wa Mikutano wa Umoja na ni Nguvu Mkoani Kisiwani Pemba.

Alisema zipo changamoto zilizojitokeza kwa baadhi ya Masheha Nchini ndani ya mchakato unaoendelea wa zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura za kulazimishwa na baadhi ya Viongozi wa Kisiasa kutoa uthibitisho kwa wafuasi wao wa kupatiwa barua itayomruhusu kuandikishwa hata kama mfuasi huyo si mkaazi wa shehia husika.

Balozi Seif alisema tabia ya baadhi ya viongozi hao wa kisiasa ya kwenda kwa sheha na karatasi ya kuzaliwa za wafuasi wao zionawapa mashaka Masheha na kushindwa kuthibitisha kwamba wananchi hao kweli ni wakaazi halisi wa shehia hizo.

Alifahamisha kwamba utaratibu wa mpiga kura unampa haki Yule mwananchi ambae tayari ameshaishi katika eneo husika kwa kipindi cha miezi 36 sawa na Miaka Mitatu ukizingatia uhamiaji halali uliothibitishwa na shehia aliyohamia na ile aliyohama.

“ Hichi kitendo cha kulazimishwa sheha kutoa idhini ya kupatiwa kibali mtu aliyehama kwenye shehia hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu na kulazimishwa apewe fursa hiyo kwa kisingizio cha kwamba yeye mzaliwa na shehia hiyo kinakaribisha vurugu zisizo na msingi wa kidemokrasia”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametahadharia wananchi kwamba mfumo wa baadhi ya watu kutafuta vyeti wa kuzaliwa kwa njia ya magendo ni kwenda kinyume na sheria na taratibu za Nchi.

Alifahamisha kwamba watu wenye tabia ya kutaka kuingia kwenye daftari la wapiga kura kwa ajili ya kujiandaa kuwachagulia Wazanzibari Viongozi wao kwenye uchaguzi Mkuu ujao si halali na itaendelea kubeba dhima dhidi yao.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewasisitiza Masheha wa Mkoa wa Kusini Pemba ambao zoezi la Uandikishaji wa Daftari la wapiga kura unaendelea kwamba Mwananchi mwenye sifa za kujiandikisha kwenye daftari hilo lazima anapatiwa haki yake hiyo.

Akizungumzia harakati za uchumaji wa zao la Karafuu Balozi Seif alisema jitihada za wananachi, Wakulima na Wafanyabiashara katika kuimarisha zao hilo ndizo zinazoipa nguvu Serikali katika utekelezaji wa majukumy yake.

Alisema miundo mbinu inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote inatokana na nguvu za Uchumi zinazotokana na zao la Karafuu pamoja na washirika wa maendeleo.

 Balozi Seif alifahamisha kwamba wapo watu wachache ambao bado wana tabia ya kutumia fursa walizonazo katika kulihujumu zao la Karafuu kitendo ambacho wananchi wanapaswa kupambana nacho kwa hali yo yote ile.

Alieleza kwamba umefika wakati kwa Wananchi kufikia pahala wakaelewa kuwa uchumi wao wa Karafuu ndio tegemeo pekee litakalowezesha nguvu za uimarishaji wa miundo mbinu mbali mbali kwa faida ya jamii yote kwa ujumkla.

“ Nimeiona Bara bara niliyoipita kutoka Chake chake hadi hapa Mkoani imeshaanza kuharibika. Wakuitengeneza ni sisi wenyewe kwa kutumia Mtaaji wetu. Sasa anapotokea Mtu kujinufaisha pekee kwa kutumia Uchumi wetu wa Karafuu ni hatari kwa Nchi”. Alitahadharisha Balozi Seif.

“ Nimefarajika ziara yangu niliyoifanya hivi karibuni nimeshuhudia na kuona jinsi Wananchi walivyohamasika kuuza karafuu zao kwenye Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC }”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Mapema baadhi ya Masheha hao wa Mkoa wa Kusini Pemba walielezea changa moto wanazopambana nazo katika harakati zao za utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Masheha hao waliishauri Serikali na taasisi zinazohusika na masuala ya uandikishaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura kuelewa kwamba wao ndio wahusika wakuu wanaoelewa na kutambua wakaazi waliomo kwenye shehia zao.

Walitahadharisha kwamba kitendo cha kupewa maamuzi wakuu wa Vituo vya uandikishaji unaweza kutoa fursa kwa watu wasiohusika wala haki za uandikishaji kwenye shehia zao kupata nafasi hizo jambo ambalo litakwenda kinyume na sheria za kidemokrasia zilizowekwa na kukubalika Nchini.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara ya kukagua Kituo cha Zimamoto na Uokozi Kilichopo Bandari na Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.

Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Kikosi hicho Kisiwani Pemba kulitumia eneo walilopewa na Shirika la Bandari kwa shughuli zao za kupambana na majanga na maafa wakati yanapotokea.

Aliueleza Uongozi wa Zima moto na Uokozi Pemba kwamba atafanya juhudi za kukutana na Uongozi unaohusika na eneo hilo kuangalia taratibu zitakazotoa fursa kwa kikosi hicho kubakia eneo hilo ili kitekeleze majukumu yake kwa utulivu na uhakika.

Mapema Mkuu wa Idara ya Zimamoto na Uokozi Kisiwani Pemba Msaidizi Kamishna Shaaban Zidi Kheir alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Kituo hicho kipo eneo hilo kwa lengo la kutoa huduma Bandari ya Mkoani pamoja na Wilaya nzima ya Mkoani.

Msaidizi Kamishna Shaaban alisema kikosi hicho kinaendelea kujipanga kutekeleza Sera za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuwa na kituo cha Zima moto na Uokozi kila Wilaya hapa Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top