Baraza Kuu la Uongozi la CUF linakutana jijini Dar es Salaam kwa kikao chake cha kawaida cha siku mbili. 

Akifungua kikao hicho kinachofanyika ukumbi wa mikutano ofisi kuu ya chama hicho Buguruni Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba amesema pamoja na mambo mengine kikao hicho kitajadili mpango wa maendeleo kwa wote ulioandaliwa na chama hicho. 

Amesema chini ya mpango huo, chama hicho kinajipanga kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, sambamba na kuimarisha viwanda vitakavyosaidia kupunguza tatizo hilo linalowakabili vijana wengi nchini. 

Amesema hali ya uchumi bado ni ngumu kwa wananchi wengi wa Tanzania, hali inayotokana na kutokuwepo mipango imara ya kukabiliana na tatizo la ajira na matumizi mabaya ya rasilimali za nchini. 

Ametaja tatizo jengine linaloukabili uchumi wa Tanzania kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma, pamoja na mikataba ya kiuchumi isiyotekelezeka. 

Akizungumzi matukio ya hujuma yanayojitokeza Tanzania, Profesa Lipumba amewaomba Watanzania kuungana kulaani vitendo hivyo bila ya kujali itikadi za aina yoyote. 

Amelilaumu jeshi la polisi na vyombo vya dola kwa kusahau wajibu wake wa kushughulikia matatizo makubwa ya kitaifa yakiwemo tatizo la dawa za kulevya, na badala yake kushughulikia masuala ya kuwadhalilisha wananchi katika maeneo tofauti ya Tanzania yakiwemo Mtwara, Arusha, Zanzibar sambamba na kuwashugulikia viongozi wa kidini. 

“Kashkashi ya Sheikh Ponda imekuwa kama ameonekana Osama Bin Laden hapa Tanzania, hii ni hatari kabisa”, aling’aka Prof. Lipumba. 

Mapema akitoa utangulizi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema jumla ya wajumbe 46 kati ya 51 wa kikao hicho wamejitokeza, na kwamba ni halali kwa mujibu wa katiba ya chama hicho. 

Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi ni kikao kikubwa cha pili cha maamuzi kikifuatiwa na kile cha Mkutano Mkuu.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top