Watendaji wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wanapaswa kuendeleza tabia waliyokuwa nayo ya kushirikiana pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi ili kufanikisha lengo lililokusudiwa na Taifa.

Nasaha hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kufutari pamoja na baadhi ya Wafanyakazi hao hapo nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Futari hiyo pia iliwajumuisha majirani wa Balozi Seif waliyozunguuka makazi yake, Kamati ya wananchi wanaoishi katika eneo la Uwanja wa ndege pamoja na baadhi ya Wawakilishi na watendaji wa Taasisi nyengine za Serikali.

Balozi Seif alisema ushirikiano wa watendaji wa Wizara hiyo ambao ndio unaosimamia shughuli za Serikali umemuwezesha yeye akiwa mtendaji mkuu wa shughuli hizo kutekeleza kazi zake kwa ufanisi.
Alieleza kwamba wafanyakazi mara nyingi wanakuwa kazini pamoja kwa kipindi mrefu katika harakati za za kimaisha za kila siku jambo ambalo wanastahiki kupendana na kushirikiana kwa vile wanaishi kama familia moja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wafanyakazi hao wa Ofisi yake kwa kazi kubwa ya kuandaa bajeti ya Wizara hiyo na hatimae kupitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Kikao cha kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara za Serikali kwa mwaka wa Fedha wa 2013 /2014.

Akizungumzia funga ya mwezi mtukufu wa ramadhani inayoendelea Balozi Seif aliwataka waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wafanyakazi hao kutekeleza ipasavyo ibada hiyo katika taratibu zilizivyowekwa na Dini.

Alisema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umekuwa kigezo kikubwa kwa waumini wa Dini ya Kiislamu ambao huwafundisha mambo mengi endapo watayaendeleza yatawajengea hatma yao njema ya baadae.

Mapema wakitoa shukrani kwa niaba ya watendaji wa Ofisi hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Khalid Salum Mohd wamemshukuru Balozi Seif kwa utaratibu wake wa kuwashirikisha watendaji wake katika futari ya pamoja.

Walisema tabia hiyo kwa kiasi kukubwa imekuwa ikiendelea kuongeza upendo baina ya Viongozi na Wafanyakazi hao sambamba na wale wananchi wanaowahudumia.

“ Hii ni tabia ya upendo kati ya Uongozi na wale wanaowaongoza ambayo hujenga udugu na ushirikiano unaoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao “. Alifafanua Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid.

Wakati huo huo Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema Vijana wa Umoja wa Vijana Chipukizi wa CCM ndio tegemezi kubwa katika kuona Taifa la Tanzania linaendelea kuongozwa katika misingi ya amani na utulivu.

Mama Asha ambae pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini “B “ alisema hayo wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana Chipukizi wa CCM Wilaya ya Kaskazini B uliofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni.

Alisema iwapo taifa halitajizatiti katika kuwaanda vijana kwa ajili ya Uongozi wa hapo baadae mifarakano inayoendelea kuandaliwa hivi sasa kwa kisingizio cha dini inaweza kujaleta balaa katika jamii hapo baadae.

Mama Asha alifahamisha kwamba mifarakano hiyo licha ya kwenda kinyume na maamrisho ya hiyo dini yenyewe lakini pia inapingana na ile azma ya waasisi wa Taifa hili ya kuwaandalia mazingira mazuri ya maamuzi wananchi kwa kuleta ukombozi.

“ Waasisi wetu walipigania kujikomboa na madhila ya wakoloni ambayo baadhi ya watu wanakuwa vibaraka vya kushawishi kurejeshwa kwa mfumo huo ambao utasababisha kuwanyima wananachi walio wengi uwamuzi wa kujiamulia mambo yao wenyewe “. Alitahadharisha Mjumbne huyo wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “.

Katika kuunga mkono harakati zao Vijana hao wa Chipukizi Mjumbe huyo wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini B Mama Asha Suleiman Iddi amechangia Shilingi Milioni 1,000,000/- kwa ajili ya Wajumbe wote 150 wa Mkutano Mkuu wa Chipukizi Wilaya ya Kaskazini B.

Mama Asha pia alikabidhi mchango wa shilingi Laki 200,000/- kwa Kikundi cha Dufu cha Kijiji hicho, Shilingi Laki 200,000/- kwa Kikundi cha maigizo pamoja na kuahidi kutoa sare kwa Wajumbe wote 150 wa Mkutano huo Mkuu wa Chipukizi Wilaya.
Naye kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alichangia jumla ya shilingi Laki 500,000/- kusaidia kufanikisha Mkutano huo Mkuu wa Vijana wa Chipukizi Wilaya ya Kaskazini “ B”.

Akitoa Taarifa fupi ya Umoja wa Vijana Chipukizi Wilaya ya Kaskazini B Mwenyekiti wa Umoja huo Ali Khamis alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya unoja huo kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa kikundi cha kujitolea kilichojikubalisha kunadi ilani ya CCM wakati wote.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top