Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amekemea tabia ya baadhi ya Viongozi wa Chama hicho kuwa na hulka ya kuwatenga Vijana ambao ndio muhimili na wenye nguvu katika kukipigania Chama hicho. 

Kauli hiyo aliitoa katika Ukumbi wa Jamuhuri Wete Pemba wakati akizungumza na vijana wa Chama cha Mapinduzi wa kikundi cha Hatudanganyiki mara baada ya kupokea malalamiko yao dhidi ya baadhi ya Viongozi wa Chama hicho Wilaya ya Wete na Mkoa wa Kaskazini Pemba. 

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema zipo kasoro ndogo ndogo zinazotofautiana za mawazo zilizopo baina ya Viongozi na Wanachama lakini haziwezi kuachwa zinaendelea kudhoofisha nguvu za Chama hicho. 

Aliwaasa wana CCM hao kujiepusha na mgawanyiko ndani ya chama ambao unaweza kuleta balaa na kitu kinachowakabili hivi sasa mbele yao ni kuhakikisha wanapanga mikakati katika kuimarisha nguvu ya chama chao kwa ajili ya ushindi wa mwaka 2015. 

Alitahadharisha kwamba hitilafu zinazojichomoza baina ya Viongozi na Wanachama wa chama hicho ni vyema zikatatuliwa na kuishia katika Vikao vya halali na kujiepusha na tabia ya kuitana majina ya ajabu ambayo hutoa mwanya wa kudhoofisha chama. 

Balozi Seif alielezea kuunga mkono vijana hao wa CCM wa kundi la hatudanganyiki Kaskazini Pemba kwa ushujaa wao wa kutetea na kuimarisha Chama cha Mapinduzi na Kuuagiza Uongozi wa CCM Wilaya ya Wete pamoja na Mkoa wa Kaskazini Pemba kufuatilia matatizo yanayowakabili Vijana hao na hatimae kuyatatua nay ale wasio na uwezo nayo kuyawasilisha kwa Uongozi wa Juu wa Chama. 

“ Mimi kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambae pia nasimamia shughuli za Serikali ya Chama Tawala nitahakikisha baadhi ya matatizo yenu Vijana nayawasilisha kwa Makamu Mwenyekiti wetu wa CCM Zanzibar ili itafutwe mbinu ya kuyatatua “. Alisisitiza Balozi Seif. 

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwapongeza wana CCM Kisiwani Pemba kwa msimamo wao wa kuendelea kukiunga mkono chama hicho. 

Alisema Wanachama wa chama hicho Kisiwani humo ni madhubuti kutokana na kutoyumba kwao licha ya mikiki mikiki wanayopambana nayo kutoka kwa kambi ya upinzani hasa katika nyakati za uchaguzi. 

“ Ushindi wa Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi Mkuu unategemea sana wana CCM wa upande wa Kisiwa cha Pemba ambao hawatetereki wala kuyumba kutokana na vitisho vya upinzani “. Alisisitiza Balozi Seif. 

Balozi Seif aliendelea kufahamisha kwamba nguvu na uhai wa Chama cha Mapinduzi mara zote unategemea jumuiya zake za Wazazi, Vijana na UWT, hivyo Vijana hao wanapaswa kuelewa kwamba wao ni tegemeo la Chama wakati wote. 

Mapema Vijana hao wa CCM wa kikundi cha hatudanganyiki wakiongozwa na Mwenyekiti wao Omar Rashid walielezea changamoto wanazokabiliana nazo kila siku katika harakati zao za kuimarisha Chama Cha Mapinduzi. 

Walisema asilimia kubwa ya changa moto hizo ambazo zimo ndani ya uwezo wa Viongozi wenyewe zimekuwa zikiwapa wakati mgumu kutokana na udhaifu binafsi uliopo kwa baadhi ya Viongozi wa CCM Wilaya na Mkoa. 

Walieleza kwamba upo ushahidi wa wazi unaoonyesha baadhi ya Viongozi wa CCM Wilaya na Mkoa kufuja mali za Chama kwa maslahi yao binafsi pamoja na kujishirirkisha katika vitendo vya rushwa wakati zinapotokea fursa za ajira kwa ajili ya Vijana hao. 

Baadaye Balozi Seif alifika katika Kijiji cha Michakaeni Chake Chake Pemba kuipa pole Familia ya Mwanaharakati wa Chama cha Mapinduzi Marehemu Bibi Fatma Omar Khatib ambae aliyefariki dunia hivi karibuni baada ya kupata ajali ya kugongwa na Gari. 

Akiifariji Familia hiyo Balozi Seif aliwataka ndugu na jamaa wa marehemu Bibi Fatma Omar Khatib kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo. 

Alisema msiba huo wa Bibi Fatma ambao utaendelea kukumbukwa katika kipindi kirefu mbali ya kuiathiri familia hiyo lakini pia umewagusa takriban wana chama wa chama cha mapinduzi wote waliopata taarifa ya msiba huo Zanzibar na bara kwa ujumla. 

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM pia alimtembelea Mzee mwanaharakati wa CCM wa miaka mingi Kisiwani Pemba Bibi Habiba Ali Hamadi hapo nyumbani kwake Mtaa wa Michakaeni. 

Bibi Habiba mwenye umri wa Miaka 70 aliwahi kupata ajali ya gari wakati wa kampeni za mwanzo za uchaguzi wa vyama vingi vya siasa ambapo CCM iliibuka na ushindi kwa kumuwezesha Dr. Salmin Amour kuiongoza Zanzibar mnamo mwaka 1995. 

Balozi Seif alimuahidi Bibi Habiba ambae hadi sasa ni Balozi wa CCM wa nyumba kumbi kwamba Uongozi wa chama cha Mapinduzi utakuwa pamoja na yeye kwa kumpatia misaada kadri hali itakavyoruhusu kutokana na mchango wake mkubwa aliyoitoa ndani ya chama hicho.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top