Mabalozi wateule watakaoiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani wamehimizwa kuitangaza Tanzania kutokana na fursa ilizonazo kwa mashirika na Taasisi za mataifa hayo ili zishawishike kutaka kuwekeza vitega uchumi vyao hapa nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Mabalozi saba wanaotarajiwa kuiwakilisha Tanzania kwenye mataifa rafiki duniani baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete hivi karibuni.

Mabalozi hao ni Balozi Liberata Mula mula anayekwenda Nchini Marekani, Balozi Wilson Masilingi Nchini Uholanzi, Balozi Modest Mero anayekwenda Geneva na Balozi Anthony Cheche anayekwenda Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo { DRC }.

Wengine ni Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk anayekwenda Umoja wa Famle za Kiarabu { UAE }, Balozi Chabaka Kilumanya atakayeanzisha Ubalozi Mpya Nchini Comoro pamoja na Luteni General Mstaafu Abdullrahman Shimbo atakayeiwakilisha Tanzania katika Jamuhuri ya Watu wa China.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vinavyopaswa kutangazwa na Mabalozi hao nje ya Nchi ili viweza kutoa fursa ya uwekezaji na hatimae kutanua soko la ajira hasa kwa vijana wasiokuwa na kazi baada ya kumaliza masomo yao.

Aliwaeleza Mabalozi hao kwamba huo ni wajibu wao wa kuhakikisha Tanzania na Zanzibar kwa ujumla inaeleweka zaidi ili zipate kuungwa mkono katika harakati zao za kujiendeleza kiuchumi na Ustawi wa Jamii.

“ Tunakutegemeeni sana wakati Mnaitangaza Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania msisahau pia kuitumia fursa hiyo Kuitangaza Zanzibar kwa vile tayari imeshajiimarisha kimiundo mbinu katika masuala ya uwekezaji hasa kwenya utalii“. Alihimiza Balozi Seif.

Alisisitiza kwamba Tanzania lazima iendelee kujienga enga katika kuhakikisha uhusiano wake na mataifa rafiki unaendelea kuimarika na kudumu kwa kipindi kirefu zaidi.

“ Napenda kukukumbusha Balozi Wilson Masilingi utakayepeperusha Bendera ya Tanzania Nchini Uholanzi uhakikishe ile heshima ya Tanzania inarejea kama kawaida baada ya kuamuliwa kufunguliwa tena Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Nchini humo “. Alitilia mkazo Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Mabalozi hao wateule kwa kuteuliwa kwao na kuwataka kuwa wastahamilivu katika kukabiliana na changamoto watakazopambana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao mpya.

Nao Mabalozi hao wateule wakiongozwa na Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Marekani Balozi Liberata Mula mula wamewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa uamuzi wao wa kuingia ndani ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambao umesaidia kuleta mapatano kati ya wafuasi wa vyama vikuu viwili.

Walisema hatua hiyo imeiweka Zanzibar katika nafasi nzuri ya Demokrasia katika Nyanja za siasa za Kimataifa hali ambayo ina muelekeo wa kuleta matumaini ya kuendelea kuungwa zaidi mkono katika harakati zake za kujiletea maendeleo.

Mabalozi hao wamependekeza kuwepo kwa vikao vya pamoja kati ya wafanyabiashara wa Zanzibar na Tanzania Bara katika kujadili fursa zinazoweza kupatikana katika nchi rafiki ili mabalozi hao wawe na urahisi wa kuratibu mawasiliano na mipango ya wafanyabiashara hao ambayo ni muhimu katika ustawi wa Jamii na Taifa kwa ujumla. 

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top