Mabenki Nchini yametakiwa kuimarisha eneo la kuhudumia wateja kwa urahisi na haraka zaidi ili kupunguza malalamiko ya wateja wakati wanapohitaji huduma za fedha ambazo huwachukuwa muda mrefu kuzipata katika matawi ya baadhi ya Benki hizo.

Tabia hiyo huonekana kufanywa na baadhi ya Watendaji wa Matawi hayo kwa kutokaa kutoa huduma katika sehemu zao za kazi na kuwapa mwanya baadhi ya watumishi wa Umma kupata kisingizio cha kutoroka makazini.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kuzindua Kituo cha kutoa huduma sambamba na uzinduzi wa huduma ya kusafirisha fedha kwa haraka { World Remit Money Transfer Servives } za Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } katika jengo la Mamlaka ya Mapato Zanzibar { ZRB } liliopo Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema wakati umefika kwa Benki za Hapa nchini kubadilika kwa kuweka malengo ya kupunguza muda wa kuhudumia wateja ambao ni wafalme katika masuala ya kupatiwa huduma.

“ Kuna malalamiko ya wateja wengi nchini kutumia muda mrefu sana wanapofika kwenye matawi ya Benki zetu. Sasa watendaji wetu umefika wakati mbadilike mara moja kwa kuweka malengo ya kuondoa usumbufu huo “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar pamoja na watendaji wake kwa kupiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma mbali mbali za Kibenki.

Alisema uanzishwaji wa huduma za usafirishaji fedha kwa haraka ni kielelezo kinachodhihirisha kwamba Benki ya Watu wa Zanzibar ni miongoni mwa Benki kongwe Nchini ambayo inapiga hatua za haraka katika utoaji wa huduma zake.

Alieleza kwamba huduma iliyoanzishwa na PBZ ya kusafirisha fedha kwa haraka kupitia mtandao wa inaternet ni huduma iliyowalenga zaidi Wazanzibari na Watanzania wanaoishi nje ya nchi waweze kutumia huduma hizo kwa kutuma fedha kwa ndugu na jamaa zao katika njia ya urahisi na uhakika.

Balozi Seif alielezea matumaini yake kwamba matumizi ya mtandao huo yataongezeka hasa kutokana na unafuu wa gharama zake kwa vile mtumaji anapaswa kuwa na mtandao wa mawasiliano ya internet ambao utamuwezesha kutuma fedha kwa haraka na kufika mara moja.

“ Jambo la kufurahisha ni kwamba kupitia huduma hizi za PBZ tunaweza kupata Taarifa kuhusu fedha ambazo zinatumwa kuja nyumbani kutoka kwa wenzetu walioko nje ya nchi ambazo pia zinaweza kutumiwa katika maeneo tofauti ikiwemo Bajeti ya Serikali na Mipango ya Maendeleo “. Alifafanua Balozi Seif.

Aliwasisitiza wananchi walioko nje ya Nchi { Diaspora } kuendelea kutuma fedha nyumbani kwa kupitia mtandao huo wa kusafirisha fedha kwa haraka jambo ambalo litakuwa chachu ya kusaidia kukuza Maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Limited Nd. Juma Amour Mohammed alisema takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia zimeeleza kwamba mfumo huu wa kusafirisha fedha kutoka ughaibuni kwenda kwa jamaa na ndugu kwenye mataifa yanayoendelea imeshafikia Dola za Kimarekani Bilioni mia 401.

Nd. Juma Amour aliyataja Mataifa yaliyofaidika na mfumo huo kuwa ni India, China, Phillipines, Mexico ambapo kwa Bara la Afrika Nigeria inaongoza kwa kupokea Dola za Kimarekani Bilioni 2.05 sawa na asilimia 9% ya pato lake wakati Kenya kwa Ukanda wa Afrika Mashariki imepokea Dola Bilioni 1.2 sawa na asilimia 3% ya pato lake.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa PBZ amewaomba Wazanzibar na Watanzania walioko ughaibuni kuitumia fursa hiyo yenye gharama nafuu kwa kuwatumia fedha jamaa na ndugu zao badala ya ule utaratibu wanaoutumia ambao hauko rasmi.

Alisema Benki ya Watu wa Zanzibar hivi sasa imefikiwa kiwango cha amana cha asilimia 40% ikishikilia nafasi ya asilimia 16% ya mabenki yaliyomo ndani ya kanda ya Afrika mashariki.

Alieleza kwamba katika kuimarisha huduma za Kibenki Uongozi wa Benki hiyo tayari imeshafungua huduma za ATM 17 ikielekea zaidi katika mtandao wa internet na Simu.

Benki ya Watu wa Zanzibar Limited imeshafungua matawi tisa pamoja na Matatu yanayotoa huduma za Kiislamu hapa Zanzibar na baadhi ya Mikoa ya Tanzania Bara tokea kuasisiwa kwake na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume Tarehe 30 Juni mwaka 1966.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top