Chama cha Wananchi CUF kimeunda jopo la wataalamu kwa ajili ya kuipitia na kuichambua rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa hivi karibuni.

Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema jopo hilo la wataalamu litakapokamilisha kazi yake, litakuwa na upeo mkubwa wa kuushauri uongozi wa chama hicho, ili kiweze kutoa tamko rasmi la chama kuhusiana na rasimu hiyo ya katiba.

Amesema kwa maoni yake Tume ya mabadiliko ya katiba imefanya kazi kubwa ya kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na hatimaye kupata rasimu ya awali ya katiba ambayo imezingatia baadhi ya matakwa ya wazanzibari.

Hata hivyo amesema rasimu hiyo bado ina kasoro nyingi ambazo zinapaswa kujadiliwa zaidi katika mabaraza ya katiba, ili kupata rasimu ya pili itakayokidhi matakwa ya wananchi, kabla ya rasimu hiyo kufikishwa katika Bunge la katiba.

Amesema bado wananchi wana fursa ya kuchangia katika rasimu hiyo kupitia wawakilishi wao watakaoingia katika mabaraza ya katiba ambapo wananchi watatoa uamuzi wa mwisho wakati wa kura ya maoni.

“Wananchi ndio waamuzi wa mwisho wa mabadiliko ya katiba, kwani baadae mutapata fursa ya kupiga kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa rasimu ya mwisho kabla ya kutiwa saini na kuwa katiba kamili”, alifafanua Maalim Seif.

Amesema pamoja na mambo mengine rasimu hiyo ya awali imezingatia kwa makini uwepo wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeundwa na nchi mbili yaanai Zanzibar na Tanzania Bara, na kwamba mara kwa mara imekuwa ikitaja washirika wa Muungano.

Mambo mengine aliyoeleza kuyakubali katika rasimu hiyo ni pamoja na kuingizwa kwa masuala ya mafuta na gesi asilia kutokuwa miongoni mwa mambo ya Muungano, mikopo na biashara za nje, ushuru wa forodha, pamoja na elimu ya juu na baraza la mitihani.

Hata hivyo amesema kuna mambo kadhaa yanayohitajika kurekebishwa katika rasimu hiyo ili kufikia lengo la kuwa na Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na jina la Muungano ambao kwa maoni yake unapaswa kuitwa “Muungano wa Jamhuri za Tanzania”, tofauti na ilivyo sasa “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.

Mambo mengine aliyoeleza kutoridhishwa nayo kwenye rasimu hiyo ni pamoja na Mambo ya nje kubakia katika orodha ya mambo ya Muungano, sarafu na benki kuu, uraia na uhamiaji pamoja na vyama vya siasa.

“Tunataka Zanzibar iwe na uwezo wa kufanya mambo yake bila ya kuingiliwa, kwa mfano iwe na uwezo wa kujiunga na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), pamoja na FIFA”, alieleza Maalim Seif.

Aidha amesema baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo kavikutolewa maelezo ya kutosha, hali inayowafanya wananchi kutoelewa mantiki halisi iliyokusudiwa, na kuiomba tume ya Mabadiliko ya Katiba kuvitolea ufafanuzi.

Miongoni mwa vipengele hivyo ni Muundo wa Muungano ambapo amesema zilizoungana tangu asili ni Tanganyika na Zanzibar, na kutaka Tume iweke wazi washirika hao wa Muungano.

Katika hatua nyengine Maalim Seif amewatahadharisha wananchi kutojihusisha na vitendo vyovyote vya vurugu na uvunjifu wa amani katika kuendelea na mchakato huo.

Kabla ya mkutano huo, Maalim Seif alifungua barza ya CUF ijulikanayo kwa jina la “msimamo” au “mtendeni Namba 2” katika kijiji cha Mfurumatonga, yenye wanachama 200.

Kwenye mkutano wa hadhara alikabidhi kadi za CUF 609 kwa wanachama wapya walioamua kujiunga na chama hicho, huku 148 kati yao wakiwa wamerejesha kadi za CCM.
 
Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Taifa, Salim Bimani, aliwakumbusha wananchi kujisajili katika daftari la kudumu la wapiga kura muda utakapofika.
Na Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top