Mataifa yanayoendelea kupiga hatua za haraka za Kiuchumi Ulimwenguni ya G. 20 yameshauriwa kuwekeza ndani ya Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki { EAC } ili kuunga mkono harakati za Kiuchumi za Mataifa hayo.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.

Rais Museveni alisema Mataifa hayo yenye muelekeo mzuri wa Kiuchumi yanaweza kuongeza nguvu zao katika kusaidia miradi ya Miundo mbinu ya Bara bara ,Mawasiliano na hata Sekta binafsi.

Alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imelenga kunyanyua maisha ya Wananchi wake kwa kuimarisha Sekta zisizo rasmi kwa vile uwezo wa Serikali hizo katika kutoa ajira hasa kwa Vijana bado ni mdogo.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alitolea mfano Taifa lake la Uganda ambalo limejizatiti katika kuimarisha nguvu za sekta binafsi ili kupunguza wimbi la vijana wengi wanaomaliza masomo yao ambao hubaki wakizurura bila ya utaratibu wa kufanya kazi.

“ Vijana popote pale walipo ndio nguvu kazi ya Taifa. Hivyo bado upo umuhimu wa kuwaandalia mazingira mazuri yatakayotoa fursa ya kuyatumikia vyema Mataifa yao “. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Museveni wa Uganda.

Akiwahutubia Viongozi hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, Waziri Mkuu wa Rwanda Bw. Pierre Damien, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar pamoja na Watendaji wao Rais Museveni alimpongeza Rais wa Kenya Uhuru Kenyata kwa kujumuika pamoja katika mkutano huo baada ya kuchaguliwa kuiongoza Kenya.

Alisema Wananachi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya wanastahiki kupongezwa kutokana na hatua yao ya kufanya uchaguzi Mkuu katika hali ya amani na utulivu.

Naye akiuhutubia Mkutano huo kwa mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Rais Mpya wa Kenya Bwana Uhuru Kenyata alisema Kenya inaendelea kujivunia kuwa mwanachama wa Jumuia hiyo ya Afrika Mashariki.

Alisema Uanachama huo unasaidia kuendeleza ushirikiano wa ujirani mwema uliopo katika kuimarisha masuala ya Kiuchumi, Forodha, Usafiri wa Anga na hata ule wa Bara bara zinazounganisha Mataifa hayo wanachama.

Bwana Uhuru Kenyata aliwaahidi viongozi wa Jumuiya hiyo kwamba Nchi yake itaendelea kuwa huru kwa mwananchi yeyote wa Jumuia hiyo kuishi au kuwajibika katika shughuli za kiuchumi Nchini mwake kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“ Lengo la waasisi wa jumuiya hii ni kuona Afrika Mashariki inakuwa moja Kiuchumi,Kibiashara, Fedha, Mawasiliano na hata Ustawi wa Jamii “. Alisisitiza Rais Uhuru Kenya.

Alieleza kwamba Wana Jumuiya ya Afrika Mashariki wana wajibu wa kufanya kazi pamoja katika kuona ushirikiano wa Jumuiya hiyo unaendelea kuwa wa kudumu milele.

Akizungumzia suala la Amani Rais Uhuru Kenyata alisema Nchi hiyo itaendelea kuunga mkono harakati za kuimarisha hali ya ulinzi ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Bara la Afrika.

Bwana Uhuru Kenyata alieleza kuwa matatizo ya ugaidi, sambamba na masuala ya uharamia yanayoikumba pembe ya Bara la Afrika yanaweza kudhibitiwa endapo nguvu za ushirikiano wa pamoja zitadumishwa ipasavyo.

Mkutano huo wa Wakuu wa Jumuiya ya Mataifa ya Afrika ya Mashariki umemteua Bwana Charles Kackson Njoroge kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Uteuzi unaotarajiwa kuanza rasmi Tarehe 9 June mwaka huu wa 2013.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top