Uongozi wa Makampuni yanayojishughulisha na masuala ya Maji Safi na salama ya Botjheng Water na Megatron kutoka Nchini Afrika Kusini umeamua kutoa fursa kwa Zanzibar katika uwekezaji wa miradi yao ya Maji na Umeme ili kuviwezesha Visiwa vya Zanzibar kutekeleza miradi yake ya Kiuchumi kwa ufanisi.

Mkurugenzi wa fedha wa Kampuni ya Maji Bwana Hardus Hattingh alieleza hayo wakati ujumbe wao ulipokutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, makazi Maji na Nishati sambamba na idara zilizohusika na miradi hiyo chini ya uenyekiti wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Hardus Hattingh alisema ujio wao hapa Zanzibar ni kuangalia mahitaji halisi ya Huduma za maji pamoja na kufikiria mbinu zinazoweza kusaidia kitaalamu kupunguza tatizo hilo.

Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Maji ya Botjheng Water ya Afrika Kusini alifahamisha kwamba Kampuni yao imelenga kusaidia Mataifa yenye matatizo ya upungufu wa huduma hizo wakiangalia zaidi Nchi za Bara la Afrika.

“ Tumefuatilia matatizo ya huduma za maji safi na salama pamoja na umeme kwenye Mataifa tofauti na kugundua kwamba tunauwezo wa kusadia kitaaluma sambamba na uwezeshaji “. Alifafanua Bwana Hardus.

Naye Mshauri wa Fedha katika Kampuni ya Umeme ya Megatron kutoka Nchi hiyo ya Afrika Kusini Bwana Johan Oelofse alieleza kwamba Taasisi yao iko tayari kuwekeza hapa Zanzibar wakati wowote kutegemea mahitaji watakayoelezwa.

Bwana Yohan alieleza kuwa Kampuni ya Megatron iko tayari na uwezo kamili wa kuendeleza miradi ya umeme ambayo mengine imeshaanzishwa katika baadhi ya Mataifa Barani Afrika.

Nao kwa upande wao Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, makazi, Maji na Nishati Nd. Al- Khalil Mirza pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Dr. Garu walisema matumizi ya huduma ya maji yataendelea kuongezeka kufuatia kutanuka kwa sekta ya uwekezaji hapa Nchini hasa katika miradi ya Utalii.

Walisema Mamlaka ya maji inahitaji kuwa na vianzio vyengine zaidi vya maji ili huduma ya maji ifikie katika asilimia ya kiwango kinachohitajika hasa ndani ya eneo la Mji ambalo bado lina upungufu wa huduma hiyo.

“ Tunaangalia zaidi kuelekeza mipango yetu katika kuhakikisha eneo la Mji wa Zanzibar ambalo limekabiliwa na idadi kubwa ya wakaazi wake linaondokana na upungufu huo wa huduma ya Maji safi na salama “. Alifafanua Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Dr. Garu.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema juhudi za ziada zinafaa kuchukuliwa katika kuona huduma za maji safi ndani ya manispaa ya Zanzibar zinapatikana kwa kiwango kinachoridhisha.

Balozi Seif alisema Mkoa wa Mjini Magharibi hivi sasa una idadi kubwa ya wakaazi wake inayofikia Laki 5.9 sawa na asilimia 46% ya wakaazi wote wa Visiwa vya Zanzibar wapatao Milioni 1.3.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Ujumbe wa Makampuni hayo ya Maji na Umeme kutoka Nchini Afrika Kusini kuitumia fursa ya upungufu wa huduma hizo hapa Zanzibar katika kuwekeza vitega uchumi vyao.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top