Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Timu ya Madaktari Bingwa wa Jamuhuri ya Watu wa China kwa umakini wake wa kutoa huduma za Kiafya katika Hospitali mbali mbali hapa Zanzibar.

Pongezi hizo alizitoa wakati wa hafla maalum ya Chakula cha Usiku alichowaandalia Madaktari hao ambao wanatarajia kuondoka Nchini Mwezi ujao baada ya kumaliza muda wao wa kutoa huduma za afya wa miaka miwili hapa Zanzibar.

Hafla hiyo fupi iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji ilifanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakifarajika kutokana na huduma nzuri wanazozipokea kutoka kwa madaktari Bingwa wa China wakati wanapofuata huduma za Afya katika Hospitali tofauti kubwa hapa Zanzibar.

Alifahamisha kwamba huduma za afya ndani ya Visiwa vya Zanzibar zimekuwa zikipanuka siku hadi siku kutokana na kuimarishwa kwa mbiundo mbinu katika sekta ya Afya kunakotekelezwa kwa pamoja kati ya Wananchi na Serikali.

Balozi Seif alieleza kuwa mfumo huo wa miundo mbinu umekuwa ukipata nguvu za ziada za misaada ya vifaa, Utaalamu pamoja na uwezeshaji unaofanywa na mashirika, wahisani na Mataifa rafiki miongoni mwao likiwemo la Jamuhuri ya Watu wa China.

“ Tumekuwa tukishuhudia kwa muda mrefu ndugu zetu wa China wanavyotuunga mkono katika masuala mbali mbali ya Maendeleo na Uchumi lakini Sekta ya Afya wameipa umuhimu zaidi Kivifaa na hata uwezeshaji “. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Watu China imekuwa ikiipatia Zanzibar Madaktari Mabingwa wa fani tofauti katika mpango maalum iliyouweka Nchi hiyo kusaidia huduma za Afya mara tu baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alisema hatua hiyo imeendelea kujenga nguvu za Kihistoria kwa wananchi na Viongozi wa Pande hizi mbili zinazoimarisha zaidi uhusiano uliopo wa kidugu wa mataifa haya rafiki.

Balozi Seif aliwahakikishia Madaktari Mabingwa hao wa Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila msaada kwa Timu za Madaktari wa chi hiyo wanaopangiwa kuja kutoa huduma za afya hapa Zanzibar.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Timu hiyo ya Madaktari Mabingwa wa China Afisa wa Ubalozi wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Bwana Zhang Zhiqiang alisema juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajengea mazingira mazuri madaktari hao zimewawezesha kutekeleza vyema majukumu yao kwa kiwango kikubwa.

Bwana Zhang alisema uungwana huo utabakia kuwa chachu ya upendo kati ya Madaktari hao na Zanzibar itakayoendelea kudumu ndani ya nyoyo zao katika uhai wote wa maisha yao.

Timu hiyo ya Madaktari Mabingwa 12 kutoka Jamuhuri ya Watu wa China ikiongozwa na Dr. Lu Jian Lian inatarajiwa kuondoka Nchini Tarehe 18 mwezi ujao wa Juni kurejea nyumbani mara baada ya kuwasili Timu nyengine mpya katika ule mpango maalum wa Wataalamu wa afya wa China kuja kutoka huduma za afya Zanzibar.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumnzo na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klepsvik hapo ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Balozi Seif aliiomba Norway kuangalia uwezekano wa kuisadia Zanzibar kitaaluma katika sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu kwa vile Nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika eneo hilo.

Alisema Zanzibar imezunguukwa na bahari pembe zote rasilmali ambayo ikitumika vyema inaweza kusaidia kutoka ajira katika kiwango kikubwa zaidi na kusaidia pia uchumi wa Taifa sambamba na kupunguza umaskini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania kwamba Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika azma yake ya kuimarisha uchumi sekta ya Uvuvi imepewa msukumo na kinachoangaliwa zaidi wakati huu ni kuwashawishi washirika wa Maendeleo na Nchi hisani kuunga mkono sekta hiyo.

Aliipongeza Norway kwa juhudi zake za kuendelea kuunga mkono harakati za maendeleo za Zanzibar kupitia Shirika lake la Maendeleo la Norad ambapo Zanzibar tayari inaendelea kufaidika na sekta za nishati na mawasiliano ya bara bara kutokana na mchango wa Taifa hilo Hisani.

Naye kwa upande wa Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klepsvik alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Nchi yake itahakikisha kwamba sekta zilizopata msaada wa Nchini hiyo zitaendelea kuungwa mkono zaidi.

Balozi Ingunn alizitaja baadhi ya sekta zilizoungwa mkono na Serikali yake hapa Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya mawasiliano ya Bara Bara Kisiwani pemba pamoja na Sekta ya Nishati Vijijini.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top