Mlezi wa wajasiri amali wa soko la Jumapili liliopo Kisonge Michenzani Balozi Seif Ali Iddi amewaomba wajasiriamali hao kuwaalika wafanyabiashara wengine kufanya biashara zao katika eneo hilo ili kuwapa fursa wananchi kupata huduma tofauti katika kipindi cha mwisho wa wiki.

Mpango huo ambao umezoeleka katika mataifa mbali mbali duniani unaweza kuwapunguzia masafa marefu wananchi na hasa wafanyakazi wa Taasisi za umma kujipatia mahitaji yao kwa wiki nzima.

 
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa ombi hilo mara baada ya kuwatembelea wajasiri amali hao ambapo pia alipata wasaa wa kununua bidhaa mbali mbali kwenye soko hilo lililoanzishwa karibu mwaka mmoja sasa.

Alisema Serikali kupitia Wizara inayosimamia ajira na uwezeshaji iliamua kutoa fursa maalum kwa wajasiri amali hao kuwapatia eneo maalum la kuuza bidhaa wanazozitengeza baada ya kulalamikia ukosefu wa pahala pa kuuzia bidhaa zao.


“ Niliamua kwa makusudi kuja kuwatembelea kuona bidhaa zenu. Lakini inaonekana harakati zenu zimepunguwa kasi sijui kwa nini ? Sasa si vibaya mngetumia fursa ya kuwaalika wenzenu kuungana nao katika kutoa huduma hizi muhimu kwa jamii “. Alieleza Balozi Seif.


Akifafanua changamoto zao zinazowakabili za ukosefu wa mitaji Balozi Seif alishauri wajikusanye kuunda vikundi vya uzalishaji vitakavyosajiliwa rasmi ili kupata mikopo kupitia Taasisi zinazohusika ikiwemo pia Wizara ya Ajira, Uwezeshaji Wananchi, Kiuchumi na Ushirika.


Hata hivyo Balozi Seif aliwapongeza wajasiri amali hao kwa jitihada zao za kujitafutia ajira na kupunguza umaskini uliowazunguuka ambapo kwa kiasi kidogo wanaweza kujisaidia kimapato.


Mapema Katibu wa wajasiri amali hao Bibi Mtumwa Ali Juma alisema wanawake hao tayari wameshajielekeza katika kuunda jumuiya itakayowasaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili.



Bibi Mtumwa alisema mfuko wa wajasiri amali hao tayari umeshakuwa na matumaini ya kifedha ambapo wako katika hatua za mwisho katika kukamilisha taratibu za usajili utakaowapa fursa ya kupata misaada pamoja na mikopo.


Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwashauri Vijana wa Maskani ya City Centre iliyopo pembezoni mwa soko hilo la Jumapili Michenzani kujiunga pamoja katika kubuni miradi itakayoweza kuwasaidia kimaisha.


Balozi alisema hayo mara baada ya kupokea changamoto zinazowakabili vijana hao ikiwemo ukosefu wa ajira sambamba na miradi ya kiuchumi ambayo husababisha ugumu wa maisha na hatimae kujiingiza katika vitendo viovu.

 
“ Mimi Ofisi yangu iko wazi wakati wowote. Cha msingi mkeshazingatia tu nini mnahitaji kufanya katika kukabiliana na maisha basi nitakuwa tayari kutafuta mbinu za kukusaidieni “. Alisisitiza Balozi Seif.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahidi Vijana hao wa City Centre kuwapatia msaada wa vifaa vya michezo ya burdani walivyoomba ili kupata wasaa wa kubadilishana mawazo wakati wa mapumziko.
 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top