Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar imepoteza fursa nyingi kwa kutokua mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiislamu Duniani “OIC”.

Amesema iwapo Zanzibar ingepata fursa hiyo ya kuwa mwanachama wa OIC ingekua mbali kiuchumi, kwa vile Jumuiya hiyo imekuwa ikichangia maendeleo ya kiuchumi kwa nchi wanachama.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo katika viwanja vya Jamhuri Jimbo la Makunduchi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliotishwa na Chama hicho.

Ameelezea kusikitishwa kwake na kitendo cha kuikosesha Zanzibar Uanachama wa Jumuiya hiyo, na kushutumu kuwa huenda ni mpango maalum ulioandaliwa wa kuipotezea Zanzibar umaarufu duniani.

“Zanzibar ndio dola kongwe zaidi katika ukanda huu wa kusini mwa Afrika, lakini tumepoteza umaarufu wetu Zanzibar”, alieleza kwa masikitiko.

Ameelezea kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya viongozi wa upande wa pili wa Muungano kwa kutoithamini Zanzibar na kuipotezea haki zake ambazo ingepaswa kuzipata.

Ametaja ujio wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman hivi karibuni pamoja na Rais Mwai Kibaki wa Kenya kufika Tanzania bila ya kupelekwa Zanzibar, kuwa ni miongoni kwa vitendo vinavyoinyima fursa Zanzibar.

“Pamoja na yote hayo, lakini Wawakilishi wa Zanzibar walitakiwa waende wakatoe maoni yao mbele ya Waziri huyo wa Oman lakini kwa masikitiko makubwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania aliyapuuza maoni na mapendekezo ya Wazanzibari”, alieleza na kuongeza kuhoji,

“Sijui inakuwaje Waziri wa upande mmoja anaweza kuiamulia nchi yenye Rais”, alisikitika.

Amefahamisha kuwa mambo yote hayo yanatokana na Zanzibar kutokuwa na mamlaka kamili, na kwamba wakati umefika sasa kwa Wazanzibari kuungana ili kuweka mustakbali mwema wa nchi yao.

Akielezea kuhusu demokrasia ya vyama vingi Maalim Seif aliwataka wananchi kuwa huru kuitumia fursa hiyo kwani ni haki yao ya kikatiba.

Amesema kila mtu yuko huru kujiunga na chama chochote cha siasa na kuwa na imani ya dini anayoitaka bila ya kuingiliwa katika maamuzi hayo.

Hatua hiyo imekuja baada ya aliyekua kaimu katibu wa vijana wa CCM Wilaya ya Kusini bw. Muaze Haji kujiengua katika chama hicho na kujiunga na CUF.

Akizungumza katika mkutano huo bw. Muaze amesema hakushawishiwa na mtu kujiunga na CUF bali ameamua baada ya kuone kuwa anachokipigania Maalim Seif kina maslahi kwa Wazanzibari wote.


Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top