Wazee wanaoishi katika nyumba za matunzo zilizopo Sebleni wanaendelea kupata faraja kufuatia jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuwajengea mazingira bora ya ustawi katika makazi yao.

Faraja hiyo inatokana na mchango mkubwa uliotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Sheni kwa kushirikiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa kuwapatia Vitanda vipya Wazee hao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika katika makaazi ya wazee hayo hapo Sebleni kukabidhi jumla ya Vitanda 28 vyenye thamani ya Shilingi Milioni 8,000,000/-.

Vitanda hivyo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyoitowa Balozi Seif wakati wa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za mwaka huu alipoizindua Nyumba moja ililofanyiwa matengenezo makubwa baada ya kuungua moto kutokana na hitilafu za umeme mwaka 2011.

Akizungumza na wazee hao uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Balozi Seif alisisitiza kwamba Serikali Kuu itaendelea kuwatunza wazee wasiojiweza kana ilani ya Chama kilichoongoza Mapinduzi ya Mwaka 1964 { ASP } kilivyoazimia.

Balozi Seif alifahamisha kwamba uongozi wa Serikali kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo ndani na nje ya Nchi utajitahidi ili kuona ustawi wa Wazee unatunzwa na kuendelezwa zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameahidi kutoa Seti moja ya Televisheni na king’amuzi kwa wazee wanaosihi kwenye Nyumba hiyo iliyofanyiwa matengenezo ili wapate fursa ya kupata Habari, Matukio pamoja na Mawasiliano yanayotokea Duniani kote.

Aliipongeza Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana ,wanawake na Watoto kwa jitihada iliyochukuwa ya kukamilicha ujenzi wa ukuta unaozihifadhi nyumba hizo za Wazee.

Alieleza kuwa hifadhi hiyo imewawezesha kuendelea kuishi kwa amani na utulivu na kuondokana na kero iliyokuwa ikiwapatapa kila mara ya kuibiwa mali na vifaa vyao.

Naye Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi aliwaahidi Wazee hao kwamba Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Sheni pamoja na yeye wataunga mkono juhudi za Viongozi hao kwa kutoa Magodoro, Mito pamoja na Mashuka katika idadi ya Vitanda vilivyotolewa.

Mapema Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohd aliwashukuru Rais wa Zanzibar na Makamu wake wa Pili kwa msaada wao huo utakaokidhi mahitaji ya Wazee hao.

Waziri Zainab alisema Wizara na Wazee hao wamefarajika na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kutekeleza ahadi aliyoitowa Balozi Seif ndani ya kipindi kifupi cha miezi miwili tuu.

“ Ahadi ni deni na mtekeleza ahadi ni muungwana. Kwa kweli uungwana huu waliotuonyesha Viongozi wetu hawa umeleta faraja iliyoje kwa Wazee wetu”. Alisisitiza Mh. Zainab Omar.

Wakati huo huo Balozi Seif akiwa pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alipata fursa ya kuangalia msingi wa jengo jipya la Skuli ya Kinduni iliyo ndani ya Jimbo hilo na kuupongeza Uongozi pamoja na Wazazi wa Skuli hiyo kwa hatua zao za kujenga jengo jengine ili kukidhi idadi ya mahitaji ya wanafunzi.

Balozi Seif katika kuunga mkono juhudi za Wananchi na Walimu hao aliagiza kupatia makisio ya gharama kwa ajili ya huduma za umeme sambamba na uchimbwaji wa Kisima cha Maji safi katika Skuli hiyo.

Mapema Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Kinduni Bibi Miza Omar Mohd alizijata baadhi ya change moto zinazoikabili Skuli hiyo ikiwa ni pamoja na uhaba wa vifaa kwa ajili ya uendelezaji jengo jipya, Maji safi pamoja na huduma ya Umeme.

Mwalim Miza alisema uongozi wa Skuli hiyo pamoja na Wazazi walifikia maamuzi ya kujenga jengo jengine jipya kutokana na ongezeko kubwa la watoto wanapelekwa kupata taaluma katika skuli hiyo.

“ Tulianza na Wanafunzi 228 wakati tulipoanzisha skuli hii. Hivi sasa tuna wanafunzi 524 kiwango ambacho tunalazimika kuwa na mikondo miwili ya wanafunzi”. Alifafanua Mwalimu Miza Omar.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top