Wananchi wa Kijiji cha kirombero wanatarajiwa kuondokana na kilio chao cha muda mrefu kilichotokana na ukosefu wa maji safi na salama kufuatia hatua za mwisho za kukamilika kwa kisima kipya cha maji na salama kilichokengwa Kijijini hapo.

Kisima hicho kimejengwa kwa msaada wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi na kugharimu zaidi ya Shilingi Milioni ishirini kinatarajiwa kuwaondoshea shida ya huduma ya maji Wananchi hao.

Katika hatua za kukamilika kwa Kisima hicho Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi Vifaa vya ujenzi ikiwa pamoja na matofali saruji na mchanga ili kuendeleza ujenzi wa Jengo litakalokuwa hifadhi ya kisima hicho.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho walioshuhudia makabidhiano hayo Balozi Seif alieleza matumaini yake kwamba kukamilika kwa kisima hicho itakuwa ni hatua kubwa kwa wananchi hao ya kupata maji yenye uhakika.

Aliwaeleza Wananchi hao kwamba tatizo la uhaba wa maji bado linaendelea kuyakabili maeneo mengi nchini Mjini na hata Vijijini, lakini Serikali itaendelea na jitihada kwa kushirikiana na nguvu za washirika wa Maendeleo kukabiliana na tatizo hilo.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope alipata fursa pia ya kutembelea ujenzi wa jengo Jipya la Skuli ya Maandalizi na baadaye kuwa ya msingi ya Kijiji cha Pangeni na kupongeza jitihada za Wananchi wa Kijiji hicho katika hatua za kuwajengea mazingira bora ya kielimu watoto wao.

Balozi Seif katita kuunga mkono juhudi za wananchi hao wa Pangeni ameahidi kuchangia nondo 15 na saruji mifuko 30 ili kuendeleza ujenzi huo ulioanza mwaka 2010 kwa nguvu za wananchi wenyewe.

Mapema Balozi Seif aliikagua Nyumba ya Walimu ya Skuli ya Upenja na kuridhika na hatua iliyofikiwa jambo ambalo limempa faraja iliyomshawishi kuahidi kusaidia hatua za mwisho za ujenzi wa kisima cha Skuli hiyo ili kiweze kutoa huduma baada ya kukamilika kwake.

Balozi Seif ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alitembelea Matawi ya CCM ya Kichungwani, Mgambo na Pangeni ili kukagua maendeleo ya uimarishaji wa Matawi hayo.

Katika nasaha zake Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Viongozi na Wana CCM wa Matawi hayo kwamba ushindi wa CCM katika chaguzi zote Nchini ni wa msingi kulingana na mazingira ya Historia ya Taifa hili.

Aliwaagiza Wana CCM Kuendelea kushikamana na kushirikiana hatua ambayo itajenga mazingira mazuri ya kuenga nguvu za uwajibikaji sambamba na kukabiliana na njama zozote dhidi ya Chama hicho.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba njama za kubaguana zinazoonekana kuchipua Nchini kwa kisingizio cha Dini zikiachiliwa zinaweza kulipeleka mahali pabaya Taifa hili.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM alikabidhi mchango wa Shilingi 500,000/- kwa ajili ya kutandaza waya kwa hduma ya umeme katika Tawi la CCM Mgambo, Hard Board kwa kukamilisha Tawi la CCM Pangeni pamoja na ndoo mbili za Rangi kwa Msikiti wa Pandeni.

Michango yote hiyo aliyoitoa iliyojumuisha pia vifaa vya Kisima cha maji Kirombero umegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni tatu na laki mbili { 3,200,000/- }.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top