Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wameaswa kuwa na tahadhari na cheche zinazoanza kupandwa miongoni mwa Jamii za kuichezea amani unaoonekana kufanywa na baadhi ya watu kwa kuendeleza tabia ya kuhujumu baadhi ya Viongozi wa Dini hapa Nchini.

Tahadhari hiyo imetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na wana CCM katika ziara yake ya kukagua harakati za utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ndani ya Jimbo la Kitope liliomo katika Wilaya ya Kaskazini “ B ”.

Balozi Seif akiwa pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mbunge wa Jimbo la Kitope alisema matukio ya hivi karibuni ya hujuma zilizopelekea mauaji na majeruhi dhidi ya Viongozi wa Dini zinapaswa kukemewa na wana CCM hao pamoja na Wananchi wote kwa ujumla.

“ Licha ya cheche hizi za matukio ya hujuma yaliyoelekezwa Zanzibar hivi sasa lakini bado Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuhubiri amani na Utulivu kama ilani yake inavyoelekeza”. Alisisitiza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba wanachama wa chama cha Mapinduzi lazima waendelee kujiepusha na ushawishi huo unaopenyezwa kwa kisingizio cha Dini ambao ni hatari miongoni mwa Jamii Nchini.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwapongeza Wanachama na Viongozi wa CCM wa Matawi ya Kitope A, Muembe Majogoo na Boma kwa jitihada zao zilizopelekea kujenga matawi yao mapya kwa kushirikiana na Viongozi wao.

Alisema inafurahisha kuona zaidi ya asilimia Tisini na Tano ya Matawi yaliyomo ndani ya Jimbo la Kitope yameshajengwa katika kiwango kinachokubaliwa ambacho kinakwenda sambamba na hadhi ya Chama chenyewe.

Aliwaagiza Viongozi na Wana chama wa Matawi yanayoendelea kujengwa ambayo tayari ameshayapatia Vifaa vya ujenzi kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo kwa wakati ili ifikapo mwaka 2015 mikutano yote ya wanachama katika kupanga safu ya Uchaguzi inafanyika ndani ya Ofisi zao mpya.

Katika ziara hiyo Balozi Seif pia alipata fursa ya kuangalia jengo jipya la Skuli ya Matetema ambalo tayari wanafunzi wa Kijiji hicho wameanza kulitumia rasmi kwa karibu wiki ya tatu sasa kuendelea na masomo yao.

Aliuagiza Uongozi wa Kijiji hicho kuanzisha Kamati ya Skuli itakayosimamia changamoto zinazowakabili ikiwemo ongezeko kubwa la idadi ya watoto Kijijini hapo.

“ Utaratibu uliopo sasa katika maeneo yetu Wananchi huanzisha miradi yao ya maendeleo na baadae kuungwa mkono ya Serikali pamoja na Washirika wa Maendeleo. Sasa anzeni jengo jengine ili kukabiliana na changamoto zilizokuzunguukeni na mimi pamoja na Wizara husika tutajaribu kusaidia kutafuta mbinu za kuunga mkono juhudi zenu mlizoanzisha”. Alisisitiza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.

Balozi Seif halkadhalika alikikagua Kituo cha Afya cha Kitope na kutoridhika na hali ya kimazingira na kuwakumbusha watendaji wake kuzingatia usafi wa mazingira yanayokizunguuka Kituo hicho .

Katika ziara hiyo Balozi Seif akakabidhi Kisima cha Maji kwa ajili ya matumizi ya Wananchi wa Kijiji cha Boma.

Akizungumza na Wananchi hao Balozi Seif alisema pamoja na hitilafu ndogo ndogo zilizojitokeza za uhaba wa maji katika Kisima hicho aliagiza kupatiwa makisio halisi ili kutafuta uwezeshaji utakaosaidia kuliondosha tatizo hilo.

Katika kuunga mkono juhudi za Wanachama hao wa CCM Balozi Seif alichangia matofali 1000, Saruji mifuko 10, Mchanga na shilingi 100,000/- za Fundi kwa kuendeleza ujenzi wa Tawi la CCM Boma pamoja na shilingi Laki 220,000/- kwa ajili ya ununuzi wa madirisha ya Tawi la CCM Muembe Majogoo.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top