Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezuia mauzo ya waya wa umeme aina ya Shaba uliokuwa ukitumiwa na Kiwanda cha Sukari Mahonda ambao tayari ulikuwa umeshauzwa kwa shilingi Milioni Mbili na Nusu { 2,500,000/- }.

Waya huo unakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 300,000,000/-.

Zuio hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari pamoja na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya maendeleo Zanzibar hapo katika ofisi za Kiwanda cha Sukari Mahonda.

Balozi Seif alisema zipo hitilafu zinazotumiwa na baadhi ya maafisa wa Serikali katika mauzo ya mali za Serikali na matokeo yake kusababisha kuitia hasara kubwa Serikali Kuu.

Amesema Mali za Serikali zimekuwa zikinunuliwa kwa gharama kubwa lakini uuzwaji wake baada ya matumizi hayalingani na thamani ya mali zenyewe jambo ambalo hutoa mwanya kwa mali hizo kuuzwa kwa bei ya chini kabisa.

“ “ Utashangaa kuona mali za Serikali hununuliwa kwa gharama kubwa lakini baadhi ya maafisa na watendaji wa serikali hutumia mwanya wa kujenga hoja ya kuuzwa mali hizo kwa kisingizio cha kuchakaa na badala yake baadhi yao kujiuzia wenyewe kwa bei wanayoitaka wao wenyewe bila ya kuzingatia taratibu zilizopo za tenda na mnada”. Alionya Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kukaa pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari kuangalia nanma ya matumizi ya waya huo ambao ulikuwa ukitumiwa na Kiwanda hicho.

Waya huo ulilazimika kufukuliwa na Uongozi wa Kiwanda hicho baada ya kubainika kuanza kuhujumiwa kwa kukatwa katwa na baadhi ya wezi kufuatia kutambulikana thamani yake katika masoko ya Kimataifa.

Mapema Mshauri wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Dr. Hamza Hussein Sabri alisema Zanzibar inatarajiwa kujitosheleza kwa Sukari ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu kufuatia uongozi wa Kiwanda cha sukari Mahonda kufanikiwa kupata washirika zaidi katika kuongeza nguvu ya kuanza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa matumizi ya Jamii.

Dr. Hamza alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Kiwanda hicho umeongeza nguvu za Wataalam kutoka Kampuni ya Biashara za Nje { Export Trade Group } ambazo matunda yake yataonekana ndani ya mwaka huu.

“ Tunaimani thabiti kwamba Zanzibar itaweza kujitosheleza kwa Sukari kufuatia uzalishaji wetu wa Sukari kuwa mkubwa utakaowezesha Tani 50,000 za miwa kuzalisha Tani 400 za Sukari safi. Hii ni sawa na Tani 40 kwa siku kiwango ambacho tunauhakika kitatosheleza kabisa”. Alisema Dr. Hamza.

Mshauri huyo wa Kiwanda cha Sukari Mahonda alifahamisha kwamba wananchi wa maeneo yanayokizunguuka kiwanda na mashamba ya miwa tayari wameshaonyesha moyo wa kusaidia kuendeleza mradi huo ambao utatoa fursa ya ajira miongoni mwa wananchi hao.

Naye Mkurugenzi wa Mashamba wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Bwana Narayani amesema taratibu za uimarishaji wa mashamba ya miwa uko katika hatua nzuri na uoteshaji miwa unatarajiwa kuanza rasmi kabla ya mwezi wa Aprili Mwaka huu.

Bwana Narayani alisema hatua za awali zitaanza kwa kujumuisha ekari 1800 zilizopo katika maeneo ya Mahonda na Upenja ambapo zaidi ya familia 5000 zinatarajiwa kufaidia kiajira kutokana na mradi huo wa uzalishaji Sukari.

Hata hivyo Bwana Narayani alieleza kwamba zipo baadhi ya changamoto ikiwemo suala la umeme wa uhakika ambalo linatafutiwa ufumbuzi kupitia washirika wa maendeleo pamoja na baadhi ya mashamba ya miwa ambayo yatahitaji kufanyiwa marekebisho kwa vile yalikuwa yakitumiwa kwa kilimo chengine.

Mkurugenzi huyo wa mashamba wa Kiwanda cha Sukari alisema kwamba mradi huo wa Sukari mahonda umetengewa Dola za Kimarekani kati ya 35 hadi 40 Milioni kuendeshea mradi.

Alisema kati ya fedha hizo shilingi za Kitanzania Milioni 65,000,000/- zitaelekezwa katika uimarishaji wa mashamba ya miwa Mahonda na Upenja ili kuwa na uhakika wa mali ghafi kabla ya kuanza kwa uzalishaji.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameelezea kufurahishwa na hamasa hiyo mpya iliyoonyeshwa na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari kwani hamu ya Serikali ni kuona Bidhaa ya sukari inazalishwa hapa Nchini.

Balozi Seif alisema uzalishaji wa sukari Zanzibar umekuwa Historia na ndoto tokea kumalizika kwa mkataba wa ubia uliokuwa ukiendeshwa kwenye kiwanda hicho kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Ile ya Jamuhuri ya Watu wa China.

“ Ukweli hii kampuni iliyokuwa imetiliana saini na Wizara ya Fedha kukiendesha kiwanda hicho cha sukari ilikuwa ikitunyima raha na tayari tulikuwa tukifikiria kuuangalia tena Mkataba huu kwa vile lile lengo lililokusudiwa limechukuwa muda mrefu sana”. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kukagua baadhi ya maeneo ya Kiwanda hicho ambayo tayari yameanza kufanyiwa marekebisho makubwa na kuridhika na hatua iliyofikiwa.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top