Serikali ya India imetenga nafasi kumi maalum za masomo kwa Wazanzibari katika azma yake ya kuendeleza ushirikiano uliopo wa kihistoria baina ya mataifa hayo mawili.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mdogo mpya wa India anayefanya kazi hapa Zanzibar Bwana Pawan Kumar wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Pawan Kumar alisema hiyo ni fursa maalum iliyopata Zanzibar mbali na ule utaratibu iliyojipangia India wa kutoa nafasi za masomo katika mpango wake wa ushirikiano kati yake na Bara la Afrika uitwao India/Afrika.

Alisema Tanzania pekee hufikia idadi ya nafasi ya zaidi ya 300 katika mpango huo unaojumuisha Mataifa ya Sudan , Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo { DRC }, Ethiopia, Eritrea, Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Balozi Pawan alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba utaratibu unaandaliwa kwa wataalamu wa Nishati wa India kutoka mafunzo maalum kwa wanawake 30 wa Vijijini Barani Afrika watakaokuwa chachu ya upatikanaji wa umeme unaotumia jua Vijijini.

Alisema Kijiji cha Kandwi kiliopo Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja kimependekezwa kuwa cha majaribio katika mradi huo kwa kujumuisha nyumba zipatazo mia moja.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza India kwa moyo wake wa kuendelea kuisaidia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Balozi Seif amesema Jamii ya Watanzania imekuwa ikishuhudia juhudi hizo za India ambazo zinaendelea kuwawezesha Wataalamu wa kizalendo kupata Taaluma katika sekta fofauti.

Alieleza kwamba Zanzibar kwa kuwa inaelekea katika kilimo cha umwagiliaji maji sio vibaya kwa India kuunga mkono kwa kutoa msukumo wa taaluma hasa kwa wale wakulima wadogo wanaotegemewa kuongeza uzalishaji lengo likiwa ni kupunguza umaskini na kujiongezea kipato zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba jamii kubwa ya wakulima tayari wamekipokea kilimo hicho lakini kinachokwamisha zaidi uendeshaji wake ni uhaba wa rasimlani ya maji inayohitaji taaluma ya kutosha.

Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri India kupitia Balozi wake huyo kuangalia uwezekano wa Nchi hiyo kutoa fursa kwa Wajumbe wa Kamati za Baraza la Wawakilishi kupata uzoefu wa Kikamati kwa kupatia mafunzo ya muda mfupi Nchini humo.

Alieleza kuwa India imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo kupitia kamati zake za Mabaraza ya kutunga sheria ambazo zimekuwa na uwezo na Uhuru kamili wa kuendesha kazi zake.

Bwana Pawan Kumar alifika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Nchi yake kushika wadhifa huo wa Balozi Mdogo wa India hapa Zanzibar. 
 
Othman Khamis Ame  
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top