Jumuiya ya Al-Rahma ya umoja wa Falme za Kiarabu yenye Makao Makuu yake Nchini Ras Al- Khaimah imekusudia kuvisaidia Vijiji vyenye mazingira magumu hapa Zanzibar katika kuvipatia huduma humimu itakayozingatia maisha ya kila siku ya mwanaadamu.

Mkuu wa Idara ya Miradi ya Misaada ya Jumuiya hiyo Mhandisi Jumah Loojab Al-Ali akiwa pamoja na baadhi ya maafisa wa Jumuiya hiyo alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Mhandisi huyo wa Jumuiya ya Al Rahma ambae yeye na ujumbe wake wapo Zanzibar kufanya ziara maalum ya kukagua baadhi ya Vijiji hivyo kwenye maeneo tofauti Unguja na Pemba alisema taasisi yao tayari imeshajizatiti kuendeleza mradi huo kwa lengo la kuwajengea mazingira bora Wanavijiji watakaobahatika kuwemo kwenye mradi huo.

Mhandisi Jumah Loojab alifahamisha kwamba miradi iliyopewa umuhimu wa kwanza katika mpango huo ni pamoja na suala la Maji safi na salama, Vituo vya Afya, Skuli, Bara bara hata kwa kuanzia kiwango cha Fusi pamoja na kuwapatia sare za Skuli Watoto yatima na wale wenye mazingira magumu.

“ Tutatoa kipaumbele kwanza katika kushughulikia suala la maji kwenye maeneo hayo tutayoanzia atukielewa kwamba maji ni uhai kwa mwanaadamu na baadaye Afya na Skuli”. Alifafanua Mhandisi Jumah Loojab.

Mkuu huyo wa Idara ya Miradi ya Misaada ya Jumuiya ya Al-Rahma ya Umoja wa Falme za Kiarabu ya Nchini Ras Al-Khaimah alisisitiza kwamba mradi huo utakaosaidia Vijiji vyenye mazingira magumu hapa Zanzibar ambao tayari umeshatengewa majeti yake maalum unatarajiwa kufanyika katika kipindi cha miaka mitano.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Jumuiya hiyo ya Al-Rahma ya Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia uratibu wa Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi ya Nchini Ras Al-Khaimah Bwana Kamal Ahaya.

Balozi Seif alisema Zanzibar bado ina Vijiji vingi ambavyo vinakabiliwa na mazingira duni ya miundo mbinu kwa ajili ya kupata huduma za Kijamii na kiuchumi kama bara bara, Vituo vya Afya sambamba na Skuli.

“ Mradi huu ambao mmeamua kujitolea kikweli kweli utaweza kuwakomboa wananchi kadhaa waliomo ndani ya vijiji hivyo ambavyo nimefarajika kuona kwamba mmepata fursa ya kuvitembelea baadhi yake”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inakaribisha Washirika wa maendeleo ndani na nje ya Nchi katika kuunga mkono harakati zake za kuwaondoshea shida wananchi kwenye maeneo yote ya Visiwa vya Zanzibar.

Balozi Seif aliutakaUjumbe huo wa Jumuiya ya Al- Rahma kwa kushirikiana na wenyeji wao kuhakikisha kwamba ziara yao ya kukagua Vijiji hivyo inavigusa zaidi vile vyenye mazingira magumu zaidi ikilinganishwa na vyengine ambavyo tayari vimeshapata muelekeo mzuri.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top