Mataifa ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Mashariki { EAC } yametakiwa kuwa makini katika mfumo na muundo mzima wa Sekta ya Mafuta na Gesi ambayo inatarajiwa kuwa muhimili wa Uchumi mpya katika ukanda huu wa Bara la Afrika.

Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein wakati akiufunga Mkutano wa Sita wa siku tatu wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu mafuta, Gesi na Maonyesho ya Taaluma ya Sekta hizo uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha {AICC }.

Dr. Shein ambaye Hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Ukanda wa Afrika Mashariki hivi sasa unahitaji kuwa na sauti ya pamoja katika muundo huo utakaowezesha Sekta hiyo kuyanufaisha Mataifa hayo Wanachama katika Maendeleo ya Kiuchumi.

Alisema Wawekezaji pamoja na Makampuni ya Kimataifa yanayojihusisha na Sekta ya Mafuta na Gesi yanaweza kushajiika na mfumo mzima wa ukanda huu kutegemea zaidi sera na juhudi za Miundo mbinu itakayowekwa na Walaamu wa Mataifa hayo.

“ Ukanda wa Afrika Mashariki umeonyesha dalili za mapema za kuwepo kwa rasilmali ya Mafuta na Gesi miaka mingi iliyopita lakini kilichokosekana ndani ya muda huo ni utaalamu wa Kuendesha Miradi inayotokana na Sekta hiyo”. Alifafanua Dr. Shein.

Alifahamisha kwamba idadi kubwa ya Wawekezaji tayari wameshaonyesha nia ya kutaka fursa ya kuwekeza katika Sekta ya Mafuta na Gesi ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Uganda na Kenya kugundulika kuwa na Mafuta na Gesi kwa Tanzania.

Aliwapongeza Viongozi na Wataalamu wa Mataifa hayo ya Afrika Mashariki kwa juhudi zao zilizosaidia kufanikisha Mikutano na vikao vilivyolenga kuimarisha Sekta hiyo mpya kwa maendeleo ya Uchumi wa Mataifa yao.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuufunga Mkutano huo wa Mafuta na Maonyesho Waziri wa Nishati wa Uganda Mh. Irin Muloni alisema uendeshaji wa sekta ya Mafuta katika ukanda wa mataifa ya Afrika Mashariki utaimarishwa ipasavyo kwa maslahi ya Mataifa hayo.Mh.

Mapema Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki { EAC } Mheshimiwa Jesca Erio amewahakikishia wawekezaji wote watakaoamua kuwekeza kwenye sekta hiyo watajengewa mazingira bora ya ushirikiano.

Mheshimiwa Jesca alisema mazingira bora ya uwekezaji ndani ya sekta ya Mafuta katika Ukanda wa Afrika Mashariki ni suala la msingi katika kufanikisha na kuendeleza uchumi wa Mataifa hayo.

Akisoma maazimio ya Mkutano huo Mhandishi Gosper alisema ipo haja kwa Mataifa hayo kufanya juhudi za ziada katika kuhakikisha Sekta hiyo inalindwa kwa vile inategemewa kubadilisha Uchumi wa Mataifa Wanachama.

Mhandisi Gosper alifahamisha pia kwamba suala la mazingira lazima litiliwe mkazo kwa lengo la kulinda rasilmali zilizopo.

Mkutano wa saba wa Mafuta na Maonyesho wa Mataifa ya Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Mashariki unatarajiwa kufanyika mwaka 2015. 
 
Othman Khamis Ame  
Ofisi ya Makamu was Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top