Jumuiya ya Jumaa Al-Majid Foundation ya Dubai imesema iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu ili kuzihifadhi katika mfumo wa kisasa.

Mkuu wa taaluma na mambo ya nje wa Jumuiya hiyo Dkt. Azzeddine Benzeghiba ameeleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani.

Dkt. Azzeddine amesema nyaraka ni kitu muhimu cha kukienzi katika kutunza historia ya nchi, hivyo taasisi hiyo itashirikiana kwa karibu na Zanzibar katika kuhakikisha kuwa inasaidia kutunza nyaraka na historia yake.

Jumuiya hiyo pia imeonesha mwelekeo wa kushirikiana na taasisi za elimu nchini zikiwemo skuli za sekondari, vyuo vikuu, maktaba na taasisi binafsi za elimu.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuna haja kubwa ya kuzihifadhi nyaraka katika mfumo wa kisasa ili kutunza historia ya Zanzibar.

Amesema hali ya utunzanji na uhifadhi wa nyaraka kwa sasa sio ya kuridhisha, hivyo ipo haja ya kushirikiana na taasisi hiyo katika kutunza nyaraka na kumbukumbu za taifa.

Kuhusu elimu Maalim Seif amesema Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika miaka ya hivi karibuni kwa kufanikiwa kuwepo kwa vyuo vikuu vitatu kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, pamoja na kuwasajili watoto wote wenye sifa ya kuanza skuli.

Kwa upande mwengine Maalim Seif amesema Zanzibar inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kutoka maeneo mbali mbali kuja kuwekeza hasa katika sekta ya utalii ambayo imekuwa ikiimarika kila mwaka.

Amesema miundombinu ya uwekezaji katika sekta hiyo imeimarika baada ya kuwepo kwa usafiri wa moja kwa moja kutoka Oman hadi Zanzibar, na kwamba serikali inaangalia uwekano wa kuwepo usafiri zaidi wa moja kwa moja utaozinganisha nchi za kigeni na Zanzibar.

Amesema tayari serikali imefanya mazungumzo na makampuni mbali mbali ya ndege yakiwemo ya Uturuki, Emirates na Anatalia la Italia, ili kuweza kuleta ndege zao moja kwa moja, na kwamba yameonesha mwelekeo mzuri.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top