Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Mifuko ya Pencheni Nchini kuwekeza katika sekta ya Kilimo pamoja na Viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa kwa lengo la kuongeza ajira hasa kwa vijana ili kuondosha ukali wa maisha na kupunguza umaskini.

Wito huo ameutoa wakati akiufungua Mkutano wa Tatu wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } unaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Mjini Arusha.

Balozi Seif alisema haifurahishi kwa Taifa hili kubarikiwa kuwa na rasilmali nyingi lakini matokeo yake malighafi ya mazao mengi yanayotokana na rasilmali hizo husafirishwa nje ya Nchi hali ambayo inasababisha Serikali kupata mapato madogo.

Alisema pamoja na kazi nzuri ya uwekezaji katika kilimo inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania lakini bado Mifuko mengine ya Pencheni ina wajibu wa kufanya jitihada za kuzuia usafirishaji huo na badala yake wanayasarifu hapa nchini ili mbali ya kuongeza thamani lakini pia kutoa ajira kwa wananchi walio wengi.

“ Ikiwa Nchi ya India imeweza kupiga marufuku kusafirisha mali ghafi kama pamba ipo haja na sisi Tanzania kufanya jitihada za makusudi kabisa ya kuzuia kusafirisha mazao yetu kwa namna hiyo” Alisisitiza Balozo Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na mikakati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii { NSSF } ya kuwekeza kwenye Viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ambao utatoa fursa zaidi kwa wakulima kupata soko la uhakika wa mazao yao.

Balozi Seif alitoa mfano wa uwekezaji huu wa NSSF ambao umetoa fursa nzuri kwa wakulima wadogo wadogo wa miwa Mkoani kagera kuvuna Tani 40,000 za miwa ambazo zina thamani ya shilingi Bilioni 1.6 hali iliyoimarisha kipato cha jamii iliyo karibu na Kiwanda cha Sukari Mkoani huo.

“ Uzuri wa Serikali kuwa na Mashirika makubwa na yenye fedha kama NSSF Ndio huu kwani shirika hili kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani limeweza kujenga Vyuo vikuu pamoja na miradi mengine bila ya mikopo ya Kimataifa”. Alifafanua Balozi Seif.

Akizungumzia umuhimu wa utafiti na elimu ya kuongeza idadi ya wanachama Balozi Seif alisema ipo haja kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufanya utafiti katika sekta isiyo rasmi ambayo mchango wake katika Uchumi wa Taifa ni mkubwa.

Alisema sheria ya marekebisho ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii nambari 5 ya mwaka 2012 bado hayajasaidia kupanua wigo wa wanachama bali kinachoonekana hivi sasa ni kwa Mifuko hiyo ikishindana kwa kubadilishana wanachama wale wale.

Alieleza kwamba ni vyema kwa Mifuko hiyo ikaweka mikakati ya makusudi ya kuongeza wanachama kupitia mabadiliko ya sheria hiyo ili kuruhusu wanachama wapya wanaojiunga na mifuko kuchagua wenyewe ule mfuko wenye mazingira mazuri ya kuvutia wanachama.

Akimkaribisha mgeni rasmi Balozi Seif Waziri wa Kazi na Ajira wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Gaudensia Kabaka alisema Tanzania imefikia vigezo saba kati ya Tisa vilivyoainishwa na Shirika La Kazi Duniani { ILO } Katika Mkataba nambari 102 kuhusu mafao ya Jamii.

Waziri Gaudensia alivitaja baadhi ya vigezo hivyo kuwa ni pamoja na Uzee, Kifo, Ugonjwa, Ukosefu wa Ajira na Uzazi ambavyo vimekuwa vikitekelezwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na ile ya Pencheni.

Hata hivyo Waziri wa Kazi na Ajira Mh. Gaudensia Kabaka alieleza kwamba bado kipo kilio kikubwa kwa wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na ile ya pencheni ambacho ni ufinyu wa kukidhi mahitaji ya mafao.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania Dr. Ramadhan Dau alisema bado zipo baadhi ya changamoto zinazozorotesha utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo.

Dr. Ramadhan Dau aliitaja moja ya changamoto hiyo kuwa ni ucheleweshaji wa ukusanyaji wa michango ya wanachama ambapo mpango maalum uko tayari kutumika wa makusanyo ya michango hiyo kwa kutumia njia ya M. Pesa.

Ujumbe wa mwaka huu wa Mkutano huo wa Tatu wa Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } Hifadhi ya Jamii Tanzania iko njia panda.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top