Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar inahitaji kujipanga ili kulinda mafanikio yaliyopatikana kutokana na mradi wa kutokomeza malaria Zanzibar.
 
Amesema mafanikio yalipatikana yameiletea sifa kubwa Zanzibar, hali inayopelekea kuigwa na nchi nyengine duniani.


Maalim Seif ameeleza hayo katika kitengo cha kudhibiti malaria Zanzibar huko Mwanakwerekwe, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya kwa upande wa Unguja.


Amesema mafanikio hayo yanapaswa kulindwa na kuhakikisha kuwa malengo yaliyotarajiwa ya kuifanya Zanzibar bila ya kuwa na Malaria yanafikiwa kwa wakati.


Kwa upande wake msaidizi meneja wa kitengo cha Malaria Zanzibar Bw. Mwinyi Msellem amesema Zanzibar imepata mafanikio makubwa ya kupambana na malaria katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambapo kwa sasa ugonjwa huo upo chini ya asilimia moja kutoka asilimia 45 mwaka 2001.


Akiwa katika Bohari kuu ya madawa Zanzibar huko Maruhubi, Makamu wa Kwanza wa Rais ameelezea kufarijika kwake kutokana na mfumo wa kisasa unaotumika wa uhifadhi na utoaji wa dawa, sambamba na usambazaji wake katika vituo vya afya Unguja na Pemba.


Amesema mfumo huo wa kutumia teknolojia ya kisasa ya kompyuta utarahisisha mawasiliano baina Wizara na vituo vya afya, pamoja na kuweza kudhibiti ubadhirifu wa dawa unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu.


Akizungumza katika ziara hiyo Mfamasia mkuu wa serikali Dr. Habib Ali Sharif amesema dawa zinaweza kuhifadhiwa katika bohari hiyo kwa kipindi cha miezi sita, na wamekuwa wakitumia mfumo wa kupokea maombi kutoka vituo vya afya kwa ajili ya usambazaji wa dawa.


Katika bodi ya chakula, dawa na vipodozi, Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa bodi hiyo ili iweze kufanya kazi zake vizuri zenye lengo la kutunza afya ya jamii.


“Hii bodi inafanya kazi kwa ajili ya kulinda afya zetu, ni vizuri basi kuipa mashirikiano ili kuweza kuwadhibiti wafanyabiashara wanaoweza kuhatarisha afya zetu kutokana na kuingiza na kusambaza bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu”, alitahadharisha Maalim Seif.


Kwa upande wake mrajis wa bodi hiyo Dr. Burhani Othman Simai amesema baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiingiza bidhaa zilizopitwa na wakati pamoja na kubadilisha tarehe za kumaliza muda, hali ambayo ni hatari kwa afya ya jamii.
 
Dr. Simai ametaja baadhi ya changamoto zinazoikabili bodi hiyo kuwa ni pamoja na kuwpo bandari zisizo rasmi, upungufu wa wataalamu pamoja na uelewa mdogo wa jamii juu ya kazi zinazofanywa na bodi hiyo.
 
Ziara hiyo pia imewashirikisha watendaji wakuu wa Wizara ya Afya wakiwemo Waziri wa wizara hiyo Mhe. Juma Duni Haji na Katibu Mkuu Dr. Mohammed Saleh Jidawi.
 
Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top