Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema watendaji wa Taasisi za Umma katika Mataifa ya Bara la Afrika wana wajibu wa kuhakikisha Utumishi bora unaendelea kuzingatiwa ndani ya Taasisi zao kwa lengo la kutoa huduma sahihi kwa Wananchi wao.

Kauli hiyo ameitoa wakati akiufunga Mkutano wa Kimataifa wa 34 wa Siku Nne wa Jumuiya ya Kiafrika ya Utumishi wa Umma na Uongozi { AAPAM } uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Wananchi waliowengi ndani ya Bara la Afrika hasa wafanyakazi wamekuwa wakilalamikia huduma duni zinazoendelea kutolewa na baadhi ya Taasisi za Umma hali ambayo huwaletea mazingira magumu ya Kimaisha.

Alisema Mataifa mengi Duniani yamekuwa yakifanya Utafiti na hatimae kubadilisha mfumo wa Utumishi wa Umma ukilenga kuwajengea maisha mazuri Watumishi pamoja na Wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Watendaji wa Taasisi zinazosimamia Utumishi wa Umma Barani Afrika wanapaswa kubadilishana mawazo, uzoefu na Taaluma ili kuona mabadiliko ya haraka yanapatikana katika sekta hiyo.

Balozi Seif Aliwataka Washiriki wa Mkutano huo wa 34 wa Kimataifa wa Jumuiya ya Kiafrika ya Utumishi wa Umma na Uongozi { AAPAM } Kuifanyia kazi Taaluma waliyoongeza katika Mkutano huo muhimu kwao na Mataifa yao.

“ Sisi kama Viongozi na Wakuu wa Taasisi zetu zinazosimamia Utumishi wa Umma katika Mataifa yetu tuelewe kwamba tunabadilika, mabadiliko ambayo yataleta sura ya mafanikio katika utoaji wetu wa huduma kwa Wananchi wetu”. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba matumaini ya Wananchi walio wengi Barani Afrika yataongezeka na kujengeka zaidi endapo utumishi bora wa watendaji wa Taasisi za umma utakuwa madhubuti.

Balozi Seif aliipongeza Kamati ya Jumuiya ya Kiafrika ya Utumishi wa Umma na Uongozi chini ya Mwenyekiti wake Bwana Abdon Agaw Jok kwa uamuzi wao wa busara wa kufikiria Kuufanya Mkutano huo hapa Zanzibar.

Alisema hatua hiyo imetoa fursa kwa washiriki wa Mkutano huo kuielewa vyema Zanzibar Kiutalii na Uwekezaji na kuwasisitiza wako huru wakati wowote katika kuitumia fursa hiyo kujifunza zaidi mazingira ya Kihistoria na biashara yaliyopo hapa Zanzibar.

Mapema Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Ombeni Sefue alisema Mkutano huo wa 34 wa Kimatifa wa siku nne wa Jumuiya ya Kiafrika ya Utumushi wa Umma na Uongozi umeshirikisha Wajumbe wasiopunguwa Mia Nne.

Balozi Sefue alisema Mkutano huo umezingatia ushiriki wa Wajumbe wengi zaidi walio Vijana ambao watakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ari na nguvu zaidi katika kipindi kirefu cha Utumishi wao.

0 comments:

 
Top