Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema uanzishwaji wa mafunzo kwa njia ya mtandao (e-learning) katika Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya Mbweni, ni hatua muhimu katika wakati huu wa sayansi na teknolojia.

Amesema utaalamu huo utawasaidia wanafunzi waliopo na wasiokuwepo chuoni katika kujipatia taaluma wanayoihitaji kwa njia za urahisi zaidi.

Akiwa katika mfululizo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya kwa upande wa Unguja, Maalim Seif amesisitiza haja kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kuongezewa ujuzi ili kupata taaluma ya kutosha itakayokidhi mahitaji ya wananchi kiafya.

Amepongeza kazi nzuri inayofanywa na chuo hicho licha ya kuwepo kwa mazingira magumu ya kazi, na kwamba watendaji wa chuo hicho wameonekana kutokukata tama kutokana na kuwepo changamoto nyingi, na kutaka taasisi nyengine ziige moyo huo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji amesema chuo hicho kimepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza majengo na dakhalia ambayo yamepunguza uhaba wa madarasa ya kusomea na sehemu za kuishi wanafunzi.

Hata hivyo amesema chuo kicho bado kinakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo upungufu wa usafiri kwa wanafunzi pamoja na kuwepo kwa uvamizi wa ardhi katika eneo la chuo.

“Mheshimiwa, mgogoro wa ardhi katika eneo hili la chuo ni la muda mrefu lakini linaonekana kuwa na gumu, kwani amri mbali mbali zimeshatolewa kusitisha ujenzi katika eneo hili lakini cha kushangana hakuna amri inayofuatwa”, alisema Duni na kuongeza

“Kibaya zaidi mtu huyu anaedai kumiliki eneo hili amethubutu hata kuvunja ukuta wetu wa chuo kwa ajili ya kuendeleza ujunzi wake ambao tayari ulikwishazuiwa Makamu wa Pili wa Rais pamoja na kuwepo kwa amri ya Mahakama.

Katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema anakusudia kuitisha kikao maalum kitakachowakutanisha wahusika wa mgogoro huo wakiwemo Wizara ya Afya, Wizara ya Ardhi pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akiwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja, Makamu wa Kwanza wa Rais amewaagiza watendaji wa hospitali hiyo kuweka utaratibu utakaotumiwa na watu wote ili kuondosha usumbufu kwa watu wanaohitaji kupatiwa huduma.

Akielezea changamoto zinazoikabili sekta ya Afya, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Mohammed Saleh Jidawi amesema wanakabiliwa na upungufu wa wataalamu hasa wa maabara licha ya kuwepo kwa vitendea kazi vya kisasa.

Mkuu wa wodi ya wazazi katika hospitali ya Mnazimmoja Dr. Mwana amesisitiza juu ya kuwepo kwa uhaba wa wafanyakazi, hali inayoweza kupunguza ufanisi katika kuwapatia huduma watu wanaokwenda kujifungua ambapo zaidi ya wazazi 40 wanaweze kujifungua kwa siku moja katika hospitali hilo.

Katika hospitali mbali mbali alizozitembelea zikiwemo Kivunge na Mwembeladu Maalim Seif ameelezwa juu ya kuwepo kwa mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Mapema akitoa taarifa fupi kuhusu hospitali ya Kivunge, daktari dhamana wa Wilaya ya Kaskazini “A” Dr. Rahma Abdallah Maisara amesema kuanzia kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu, jumla ya wagonjwa 44,650 wamepatiwa huduma mbali mbali katika hospitali hiyo, kati yao asilimia 53.27 ni watoto chini ya miaka mitano.

Amesema asilimia 40 ya wagonjwa waliofikishwa katika hospitali hiyo walikabiliwa na matatizo ya kifua, asilimia 12 maradhi ya kuharisha ambapo matatizo mengine makuu ni pamoja na masikio, pua na koo, pamoja matatizo ya ngozi na macho.

Kaimu muunguzi mkuu wa hospitali hiyo Dr. Sharif Haji, amesema moja kati ya mafanikio wanayojivunia ni kuwepo na “insenereta” ya kuchomea taka za hospitali ambapo Makamu wa Kwanza wa Rais aliwataka kuangalia uwezekano iwapo taka za hospitali kuu ya Mnazimmoja zinaweza kuhamishiwa huko kwa ajili ya kuchomwa.

Maalim Seif pia alitembelea kituo cha Afya Kendwa ambacho ni cha mtu binafsi, na kuelezea kufarajika kwake kutokana na maendeleo mazuri na huduma bora zinazotolewa na kituo hicho.

Mganga msaidizi wa kituo hicho Dr. Hawa Kivembele amesema kituo hicho kimekuwa kikitoa huduma bila ya malipo kwa wananchi wa Kendwa, Kilindi pamoja na maeneo jirani.

Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top